Header Ads

Mtoto hajui KKK mwalimu mkuu kazi huna -Manyanya.


NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya amesema kuanzia mwakani serikali itawafukuza kazi walimu wakuu wa shule zote za msingi ambazo wanafunzi wake wa Darasa la Tatu watashindwa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Alitoa kauli hiyo jana wilayani Bagamoyo wakati akipokea madawati 1,000 kutoka kwa Kampuni ya mafuta ya Total yenye thamani ya Sh milioni 78 kwa ajili ya shule 10 za msingi za Bagamoyo na Dar es Salaam.
Manyanya alisema hatua hiyo itawezesha kuboresha elimu na pia kuongeza uwajibikaji kwa walimu katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu stahiki na kwa wakati unaotakiwa.
Alisema katika hali ya kawaida wanafunzi wanapaswa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kuanzia ngazi ya chekechea na wawe mahiri katika masomo hayo wafikapo Darasa la Tatu.
“Ni fedheha unamkuta mwanafunzi wa darasa la tatu hajui kusoma kwa nini? Lazima kuna uzembe ma hali sasa hili ni agizo na utekelezaji wake unaanza… tutapita huko kwenye mashule kukagua hili, tukibaini wapo wanafunzi hawajui hizi KKK hatuna sababu ya kuendelea na huyo mwalimu mkuu.
“…Tutamwambia atupishe akafanye shughuli nyingine, lazima walimu wawajibike,” alisema Manyanya baada ya kuwapa karatasi wasome na kuhesabu baadhi ya watoto wa shule za msingi waliokuwepo kwenye hafla hiyo na kusema elimu bora ni pamoja na kujua kusoma, kuandika, kuhesabu na kuelewa.
Naibu Waziri huyo pia aliipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia katika elimu hasa suala la madawati, ujenzi wa mabweni huku akisema taifa lina upungufu wa madawati 1,349,090 ambayo gharama yake ni Sh bilioni 182.1 hivyo aliwaomba wadau wa elimu kuchangia.
Akizungumza kabla ya kukabidhi madawati hayo, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Total, Jean-Christian Bergeron alibainisha kwamba kwa miaka mitatu kampuni yake imechangia madawati 3,000 yenye thamani ya Sh milioni 234 ambapo wanafunzi 9,000 wamenufaika nayo.
CHANZO:HABARI LEO

No comments