Header Ads

NI WIKI NGUMU WANAOWANIA URAIS DODOMA.

WAKATI uhai wa Bunge la 10 la Tanzania utamalizika rasmi kesho kutwa, ambapo litavunjwa na Rais Jakaya Kikwete, tukio lingine zito linatarajiwa kuutikisa mji wa Dodoma wiki hii.
Ni tukio la kupatikana kwa mgombea wa Urais wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, hivyo kuhitimisha mbwembwe, fitna na tambo za kila aina katika medani za siasa, ambazo Watanzania wamezishuhudia kabla na hata wakati wa uchukuaji fomu za kuomba ridhaa ya chama kuwania nafasi hiyo.
CCM iliyovutia wagombea 42, wanne kati yao wakishindwa kurejesha fomu ya kuwania kumrithi Rais Kikwete, kinatarajiwa kufanya uteuzi wa mgombea wake wa urais Jumapili wiki hii, ikiwa ni siku mbili baada ya kumteua mgombea wa Zanzibar.
Kwa sasa, wabunge mawazo yao hayapo bungeni, ushahidi wa hayo ni wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini Jumanne iliyopita walipokuwa wakipinga miswada ya mafuta na gesi isiwasilishwe bungeni kwa maelezo mawazo yao yapo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na wana mgogoro wa utulivu wa mawazo na fikra.
Miswada iliyokuwa ikipigiwa kelele, ambayo hata hivyo ilisomwa juzi, huku wabunge wa upinzani wakitolewa nje kutokana na kufanya fujo ni Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015,
Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015. Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mbunge wa Ubungo John Mnyika (Chadema), alisema ingawa wabunge wao zaidi ya 46 wametolewa nje na kusimamishwa wasihudhurie vikao vya Bunge, wameanza kuwaita wabunge wengine waliokuwa majimboni waingie bungeni kuanzia leo ili kuendelea kupambana kuhusiana na miswada wanayoilalamikia.
Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage (CCM), alisema juzi mjini hapa kwamba Bunge linaisha na wabunge wanarejea majimboni kwa kila mmoja kuvuna alichopanda. “Miaka yetu mitano imeisha, Alhamisi Rais anavunja Bunge, hivyo kuanzia Jumatatu (leo) tunamalizia wiki ya mwisho na kila mtu atajua amevuna nini,” alisema Rage.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, baada ya kumalizika mjadala wa miswada ya mafuta na gesi leo, shughuli hizo zitaendelea Jumatano, ambapo Muswada wa Sheria ya Tume ya Walimu utawasilishwa.
Bunge la bajeti lililoanza Mei 12 lilitarajiwa kumalizika Juni 27, lakini liliongezewa siku kutokana na miswada mbalimbali ya sheria iliyokuwa imewasilishwa. Miswada hiyo ukiacha ile ya gesi na walimu ni Muswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Benki ya Posta wa Mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Masoko ya Bidhaa wa Mwaka 2015.
Kwa upande wa CCM, joto la atakayerithi viatu vya Rais Jakaya Kikwete limezidi kupanda, ambapo wapambe wa wagombea na baadhi ya wajumbe wa vikao vya CCM kama vile Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mkutano Mkuu wameanza kuwasili kwa wingi mjini hapa.

Vyumba katika hoteli mbalimbali pamoja na nyumba za kulala wageni ni bidhaa adimu mjini Dodoma, kwani tayari CCM imechukua sehemu kubwa ya hoteli na nyumba hizo kwa ajili ya wajumbe wake wa mkutano mkuu.HABARI LEO.

No comments