Header Ads

MTIKILA:UKAWA WAMEPOTEA NJIA.


MWENYEKITI wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila (pichani), amesisitiza kuwa yeye ndiye mwanzilishi wa umoja wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kwamba malengo ya awali ya umoja huo ni tofauti na ya sasa.
Alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari , jijini Dar es Salaam jana. Alidai Ukawa anayoiona sasa haiko kwa ajili ya kutafuta ukombozi wa Watanganyika, zaidi ya kutafuta kura katika uchaguzi mkuu.
Mchungaji Mtikila alidai kuwa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi , vimekuwa wasaliti tangu mwaka 1993 yeye alipoanzisha wazo la kudai Serikali ya Tanganyika. Aliwataka wananchi wasikubali kudanganywa na Ukawa, badala yake wakipigie kura chama chake cha DP, ambacho alidai kipo kwa ajili ya kuwapatia Watanzania ukombozi wa kweli.
Kauli ya Mtikila iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Constantine Akitanda aliyesema Ukawa wanafanya ujambazi wa kisiasa. Alisema haiwezekani mtu anayetuhumiwa kwa makosa mengi halafu umoja huo ukamsimamisha kuwa mgombea wao wa urais.

Aidha, Mtikila alisema kwa sasa wanasheria wa chama chake, wanaandaa nyaraka za kuwawekea pingamizi baadhi ya wagombea urais kutokana na kutokuwa na sifa, hasa kwa kuwa na tuhuma za ufujaji mali za umma na wizi.HABARI LEO.

No comments