Header Ads

Polisi Watatu Wafa Ajalini Msafara wa Rais Magufuli.


Askari polisi watatu wamefariki dunia na wengine wawili wamejeruhiwa baada ya gari lao lililokuwa kwenye msafara wa Rais John Magufuli kutoka Singida kwenda Dodoma, kupasuka tairi na kupinduka.

Rais Magufuli alikuwa mjini Singida alikokuwa amekwenda kushiriki maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM.

Hiyo ni mara ya pili kwa askari kufariki wakiwa kwenye msafara wa Dk Magufuli baada ya aliyekuwa akiongoza msafara wake wakati wa kampeni kugongana na dereva bodaboda katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.

Askari huyo alikuwa kwenye pikipiki maalumu iliyokuwa ikiongoza msafara wakati Dk Magufuli akitoka katika Hospitali ya Lugalo kuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka alisema ajali hiyo ilitokea saa 9.40 alasiri, katika Kijiji cha Isuna, Wilaya ya Ikungi mkoani humo baada ya moja ya matairi ya gari hilo kupasuka na dereva kushindwa kulimudu.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Mkaguzi Mwajelo, Sajenti Elias Mrope na Sajenti Gerard.

Waliojeruhiwa ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Singida (RCO), Peter Majira (50
na PC Charles Simon (34) ambao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.

Gari hilo lililopata ajali ni lile lililokuwa limetangulia ili kufagia barabara kabla ya msafara wa Rais, likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani cha mkoa huo.

Sedoyeka alisema miili ya askari hao imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya mkoa huo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Kitundu Jacks alisema hali za majeruhi waliofikishwa kwenye hospitali hiyo zinaendelea vizuri.

“Mrope ndiye aliyeletwa akiwa kwenye hali mbaya, alikuwa amevunjika mbavu na mkono na akafa mara tu baada ya kufikishwa hospitalini hapa. Majeruhi wengine wamepata michubuko na wanaendelea vizuri,” alisema.  

No comments