Header Ads

Magufuli amburuza Lowassa urais 2015.

magufuliDk. John Pombe Magufuli

HUKU mchuano wa kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao ukionekana kuwahusu zaidi Dk. John Magufuli kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa muungano wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), tathmini imeakisi matokeo yalivyo hivi sasa.
10.Lowassa akizungumza jambo.Edward Ngoyai Lowassa.
Uchunguzi uliofanywa na Timu ya Uwazi Mizengwe hivi karibuni na kuihusisha mikoa yote ya Tanzania kwa kuwahoji zaidi ya wananchi wa kawaida wapatao hamsini kwa kila mkoa, umeonesha kuwa Dk. Magufuli amemburuza Lowassa kwa zaidi ya asilimia 20.
Maelekezo kutoka chumba cha habari makao makuu Dar es Salaam, yaliwaagiza wawakilishi wetu kwenye mikoa yote kama ifuatavyo kwa lengo la kupima upepo wa kiasa ulivyo na matarajio ya matokeo ya uchaguzi yalivyo endepo uchaguzi ungefanyika kipindi hiki.
“Nadhani unafahamu upepo wa kisiasa ulipofikia, naomba ufanye uchunguzi kwa kuwahoji watu wasiopungua hamsini ambao hawatoki kwenye vijiwe vya vyama vya siasa, swali la kuwauliza ni je ikiwa leo ungefanyika uchaguzi wangemchagua nani kati ya Magufuli na Lowassa?” Mbali na hilo, muongozo uliwataka wawakilishi kuacha kuuliza watu kwenye eneo moja na badala yake kuzunguka sehemu mbalimbali za mkoa na kufanya tathmini ya jumla kabla ya kuwasilisha ripoti zao za uchunguzi ambapo ripoti ya kila mkoa ilikuwa kama ifuatavyo.
ARUSHA- LOWASSA 80%, MAGUFULI 20%
Ripoti ya mwakilishi wetu kutoka Arusha imeonesha kuwa mgombea kupitia Ukawa, Lowassa ameongoza kwa kukubalika na wananchi wa eneo hilo kwa asilimia 80 huku Dk. Magufuli akipata asilimia 20 ya kura huku sababu ikitajwa kuwa mkoa huo umekuwa wa mageuzi na kwamba ni ngome ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako Lowassa ni mwenyeji wa eneo hilo.
DAR ES SALAAM- LOWASSA 30%, MAGUFULI 70
Taarifa za uchunguzi wetu zilionesha kuwa Magufuli anakubalika zaidi katika ukanda huu wa pwani kwa asalimia 70 na kumwachia Lowassa asilimia 30 huku sababu za ushindi wa mgombea huyo wa CCM zikielezwa kuwa ni eneo ambalo chama hicho tawala kimeota mizizi na kwamba sehemu kubwa ya viongozi wa chama wanaishi mkoani hapa.
DODOMA- LOWASSA 40%, MAGUFULI 60%
Sababu ambazo ziliainishwa na mwakilishi wetu ambazo zimempa ushindi mgombea wa CCM ni kwamba miaka nenda rudi mkoa huo umekuwa ukichukuliwa kuwa ni makao makuu ya serikali na kwamba wananchi wake wengi wamekuwa watiifu kwa serikali ya CCM na hivyo kuwa vigumu kumchagua Lowassa kwa kura nyingi.
GEITA-LOWASSA 50%, MAGUFULI 50%
Kwa mujibu wa uchunguzi wa timu yetu, ripoti imeonesha kuwa wagombea hao wawili wanaweza kupata ushindi unaolingana kutokana na kwamba sehemu kubwa ya mjini kuna wafuasi wengi wa Chadema ambao ni rahisi kumuunga mkono Lowassa huku wakazi wengi wa vijijini wakiwa ni wafuasi wa CCM ambao kura zao wamezielekeza kwa Magufuli.
IRINGA-LOWASSA 20%, MAGUFULI 80%
Upepo wa kisiasa katika Mkoa wa Iringa umeonesha kuwa amshaamsha ya upinzani haijashika kasi maeneo mengi hivyo kutoa nafasi kubwa ya ushindi kwa Magufuli ambaye wengi walimtaja kuwa ni mchapakazi anayeweza kuleta mageuzi nchini.
KAGERA- LOWASSA 60%, MAGUFULI 40%
Tathimini imeonesha kuwa Lowassa anakubalika kwa kiwango fulani katika maeneo mengi kutokanana uchapa kazi wake na kwamba vuguvugu la mageuzi katika maeneo mengi ya mjini limechangia kupata kura nyingi zaidi ya mgombea wa CCM.
KATAVI- LOWASSA 29%, MAGUFULI 71%
Hali ya kisiasa mkoani Katavi haijatulia kuna maeneo ambayo upinzani una nguvu kuliko CCM, lakini hata hivyo, katika siku za hivi karibuni wakazi wengi wamekuwa na mapenzi na chama tawala hasa baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye anatoka eneo hilo kuchaguliwa kuwa waziri mkuu.
KIGOMA-LOWASSA 45%, MAGUFULI 55%
Awali mkoa huo ulionekana kuwa ni wa mageuzi ya kisiasa na kufanikiwa kupata majimbo mengi kwenye uchaguzi, lakini siku za hivi karibuni mgogoro baina ya Chadema na Zitto Kambwe (kiongozi mkuu wa chama kipya cha upinzani cha ACT – Wazalendo), kukihama chama chake kumepunguza nguvu ya Chadema katika mkoa huo na hivyo kufanya uwiano wa kura baina ya CCM na Ukawa kuwa si wa kupishana sana.
KILIMANJARO-LOWASSA 83%, MAGUFULI 17%
Mkoa huu uko Kanda ya Kaskazini ambako ndiko anakotoka Lowassa, tathmini inaonesha kuwa kiongozi huyo anayegombea kupitia Ukawa anaweza kupata kura nyingi ukilinganisha na Magufuli ambaye hata hivyo chama chake katika maeneo mengi hakina nguvu na kwamba kura atakazopata zinatokana na uchapakazi wake mzuri.
LINDI, MANYARA, MARA MBEYA, MTWARA LOWASSA 70%, MAGUFULI 30%
Katika mikoa hii Lowassa ameongoza kwa kiwango kikubwa cha kura kutokana na vuguvugu la mageuzi katika mikoa hiyo huku Lindi na Mtwara ikitajwa kuwa mgombea huyo atapata kura nyingi za wananchi wa ukanda huo ambao wengi wanatajwa kupoteza mapenzi na chama tawala kutokana na vurugu za gesi zilizosababisha watu kunyanyaswa na vyombo vya usalama.
MWANZA, SHINYANGA, NJOMBE, RUKWA, MOROGORO, LOWASSA 25% MAGUFULI 75%
Mwanza na Shinyanga, Magufuli anatajwa kupata uungwaji mkono maeneo mengi, suala la ukabila linanogesha wingi wake wa kura kutokana na Wasukuma wanaoishi maeneo yao kupenda kumuunga mkono mtu wanayeamini ni mwenzao na kwamba Mikoa ya Rukwa na Njombe ni ngome ya CCM, hivyo kutisha kuwa mtaji wa mgombea huyo wa chama tawala.
PEMBA KASKAZINI NA KUSINI, LOWASSA 98%, MAGUFULI 2%
Miongoni mwa maeneo ambayo Magufuli anaweza kupoteza kura nyingi ni kwenye mikoa hii miwili ambayo ni ngome ya Chama cha Wananchi (Cuf) ambacho ni chama mshirika wa Ukawa anakogombea Lowassa, wakazi wengi wa maeneo haya watamuunga mkono mgombea wa upinzani ili watimize ndoto zao za kuleta mageuzi ya kisiasa wanayoyahitaji kwa miaka mingi.
ZANZIBAR KATI/ KUSINI, UNGUJA KASKAZINI NA MAGHARIBI, LOWASSA 25%, MAGUFULI 75%
Mikoa hiyo inaweza kumpa kura nyingi Magufuli kwa mujibu wa tathmini yetu kutokana na wakazi wengi wa maeneo hayo kuwa wafuasi wa CCM lakini pia ni watu wenye asili ya Bara na hasa Mikoa ya Tabora na Mwanza, hivyo ni rahisi kwa mgombea wa CCM kupata kura nyingi zaidi ya mpinzani ambaye chama  chake hakina nguvu sehemu hiyo.
SIMIYU, TABORA, TANGA, SINGIDA, LOWASSA 40% MAGUFULI 60%
Kiasili mikoa hii imekuwa ngome ya chama tawala hivyo itakuwa rahisi sana Magufuli kupata ushindi hata hivyo, Lowassa anatajwa kubebwa na uchapakazi wake na kwamba wananchi wanaweza kumpa kura kwa sababu wanaamini kuwa anaweza kuwaletea maendeleo ambayo wameyakosa kwa miaka mingi chini ya utawala wa CCM.
TATHMINI YA JUMLA
Tathmini ya jumla inaonesha kuwa endapo uchaguzi ungefanyika leo basi Magufuli angevuna asilimia 60 ya kura dhidi ya Lowassa.
Hata hivyo, kwa matokeo hayo hayajajumuisha kampeni za uchaguzi ambazo kwenye uchaguzi huweza kubadilisha matokeo kutoka hasi kwenda chanya na hivyo kuufanya utafiti huu kuwa mwanzo wa tathmini za awali kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Magufuli atakuwa na kibarua kigumu cha kukabiliana uso kwa macho na waziri wake mkuu wa  zamani Lowassa ambaye hivi karibuni aliipa kisogo CCM na kujiunga na Ukawa kama mgombea urais.

No comments