Header Ads

Watuhumiwa 50 wizi wa magari wanaswa


                                    Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imebaini mtandao wa wezi wa magari baada ya kukamata watu 50 sanjari na kupata magari 24 yaliyoibwa na kusafirishwa kwenda kwenye baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari kwamba, magari hayo yamekuwa yakiibwa kwa kutumia mbinu mbalimbali, ikiwemo funguo bandia na kisha kubadili chesisi.
Alitaja mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga na Kagera kuwa sehemu ambazo magari hayo ya wizi yamekuwa yakisafirishwa kwenda kufichwa kabla ya kuuzwa kwa watu mbalimbali.
Wakati baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa jijini Dar es Salaam wakiwa safarini kusafirisha magari hayo ya wizi, mengine yamekutwa kwenye maeneo hayo yakiwa yameshauzwa.
Sirro, ambaye alikuwa akizungumzia operesheni za usalama zinazoendelea mkoani Dar es Salaam, alitaja baadhi ya watuhumiwa pamoja na namba za baadhi ya magari yaliyopatikana baada ya polisi kufuatilia.
Alisema Februari 15, mwaka huu, mtuhumiwa Charles Simon (34) mkazi wa Mabibo ambaye ni dereva teksi, alikamatwa maeneo ya Kimara akidaiwa kusafirisha gari la wizi aina ya Fuso kwenda mkoani Mwanza.
“Magari wanayoyaiba, wamekuwa wakiyapeleka mafichoni katika mikoa ya Kanda ya Ziwa hasa Mwanza, Geita, Shinyanga na Kagera,” alisema Kamanda Sirro. Alitaja tukio lingine ni la Februari 15 mkoani Shinyanga katika eneo la Magereji ambako kamanda alimtaja mtuhumiwa Isack Kahwa (35) kuwa alikutwa na gari ya wizi iliyobainika mmiliki wake ni mkazi wa Tabata Segerea, Dar es Salaam, Erick Senzotz.
Kamanda alimtaja mtuhumiwa Kahwa kuwa ni Mkazi wa Ndala na fundi magari. Gari hilo linalodaiwa kuwa ni la wizi mali ya Erick, ni aina ya Toyota IST yenye namba T428 CYV rangi nyeupe. Inadaiwa mtuhumiwa huyo alikiri kuuza magari mengine.
Magari mengine ya wizi ambayo yalishauzwa ni Toyota Noah yenye namba T948 DCP, iliyokamatwa wilayani Mbogwe katika Mji wa Masumbwe mkoani Geita; likiwa limeuzwa kwa Sadiki Masele. Kwa mujibu wa kamanda, upelelezi umebaini kuwa gari hilo liliibwa maeneo ya Kimara, Dar es Salaam likiwa na namba ya usajili T799 DEU.
Kamanda alisema magari mengine yaliyokamatwa ni lenye namba za usajili T702 CMS Toyota Hiace iliyokamatwa Kahama akiwa nayo Victor Malya (38). Nyingine ni Toyota Noah yenye namba T419 iliyokamatwa Shinyanga Madukani akiwa nayo Adrian Jackson (45).
Magari mengine yaliyoibwa Dar es Salaam na maeneo yalikokutwa kwenye mabano ni Toyota Carina TI namba T185 BHK (Kandoto, Shinyanga), Toyota Noah T227 CNB (Shinyanga), Toyota Noah T445 CEN (Shinyanga), Toyota Noah T481 CFU, T778 CPB Toyota Noah.
Mengine yaliyoibwa Dar es Salaam kwa nyakati tofauti na kukutwa mkoani Shinyanga ni T289 CPP Toyota Noah , T369 CRM Toyota Verossa, T270 DBX Toyota Noah, T965 BLG Toyota RAV4, T462 CMA Toyota IST, T331 Toyota RAV4, T793 BHB Toyota Noah, T859 DCZ Fuso, T227 CKQ Toyota IST, T334 CCY Toyota Spacio, T556 CTX Toyota IST na T437 BMJ Toyota Carina.
CHANZO:HABARI LEO

No comments