TANGAZO KWA UMMA
JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI
WA JAMII
|

TAARIFA KWA UMMA.
TAHADHARI YA UGONJWA WA NIMONIA INAYOTOKANA
NA CORONA VIRUS
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
inapenda kutoa tahadhari ya ugonjwa wa nimonia inayotokana na kirusi kiitwacho
Corona virus. Mnamo tarehe 21 Mei 2015, Wizara ilipokea taarifa kutoka Shirika
la Afya Duniani (WHO) juu ya kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa wa Nimonia unaosababishwa
na kirusi cha “Coronavirus”, Korea ya
Kusini.
Ugonjwa huu unaenezwa na kirusi
kiitwacho “Middle East Respiratory
Syndrome Coronavirus (MERS Cov).” Dalili kuu za ugonjwa huu ni homa kali,
kukohoa na kushindwa kupumua kwa ghafla, na hatimaye kupata Nimonia. Dalili
nyingine ambazo zinaweza kutokea ni pamoja na kupata maumivu makali ya tumbo
pamoja na kuharisha. Kipindi kati ya kupata maambukizi mpaka
kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 10. Ugonjwa huu hutibiwa
kufuatana na dalili zilizojitokeza. Mpaka sasa hakuna chanjo maalum kwa ajili
ya ugonjwa huu.
Virusi hivi, kutokana na tafiti
zinazoendelea hubebwa na wanyama hususan ngamia na tafiti hizi zimeonyesha
uwepo wa virusi hivi kwenye ngamia katika nchi za Egypt, Oman, Qatar na Saudi
Arabia. Mara mgonjwa apatapo ugonjwa huu, uambukizo kwenda kwa mtu mmoja
hutokea iwapo mtu huyu atakuwa karibu na mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na
ugonjwa huu na kugusa majiimaji au makamasi hasa wakati wa kukohoa au kupiga
chafya. Vilevile uambukizo huweza kutokea iwapo mtu akigusa mazingira ambayo
yamechafuliwa na majimaji au makamasi ya mgonjwa aliyedhibitishwa na ugonjwa
huu.
Ugonjwa wa Corona virus uligundulika
kwa mara ya kwanza mwezi Septemba 2012 katika nchi za Mashariki ya kati huko
Saudi Arabia. Ugonjwa huo umeendelea kusambaa katika nchi za Mashariki ya kati
zikiwemo za Jordan, Qatar, na Falme za
Kiarabu (UAE). Katika bara la Ulaya, ugonjwa huu umethibitishwa kutokea nchi za
Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza na barani katika nchi ya Tunisia. Ugonjwa huu
umeendelea kuwepo kwenye nchi hizi kwa kiwango kidogo kuanzia mwaka 2012 hadi
Aprili 2015.
Ongezeko la ugonjwa huu limejitokeza zaidi kuanzia tarehe 20 Mei, 2015
katika nchi ya Jamhuri ya Korea. Hadi tarehe 20 Juni, 2015, watu 167 walikuwa wamethibitishwa
kuwa na ugonjwa huo wa nimonia ya Corona Virus na 24 kupoteza maisha. Vile vile
nchi za Thailand na China kumekuwa na mgojwa mmoja kila nchi.
Hadi sasa hakuna mgonjwa yoyote
aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Corona virus hapa nchini. Kwa
kuwa magonjwa hayatambui mipaka ya nchi ni vyema tuchukue tahadhari dhidhi ya
Ugonjwa huu.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
imeandaa mikakati ya kuzuia ugonjwa huu
usiingie hapa nchini ikiwa ni pamoja na;
- Kuongeza
kasi ya ufuatiliaji wa magonjwa (Surveillance)
hususan katika vituo vitano maalum vilivyopo nchini vinavyofanya
ufuatiliaji wa magojnwa ya neumonÃa (Influenza
sentinel surveillance sites).
- Kuongeza
kasi ya ufuatiliaji kwa vituo vya
kutolea huduma kote nchini. Aidha Wizara imeagiza kupitia waganga wakuu wa
mikoa kutoa taarifa /ongezeko la wagonjwa
watakaoonyesha dalili za ugonjwa huo hususan kwa wagonjwa ambao
wamesafiri kwenye nchi ambazo zina ugojnjwa huu. Ainisho sanifu (Standard
case Definition) imetolewa kusaidia mtaalamu wa afya kuweza kutambua
ugonjwa huu. Aidha kasi hii ya ufuatiliaji inaangalia iwapo kuna ongezeko
la Nimonia kali au mafua kulinganisha na majira ya wakati huu kwa miaka
mingine.
- Kuongeza
kasi ya ufuatiliaji wa ugonjwa huu maeneo ya mipakani hususan kwa wasafiri
watokao nje ya nchi hususani watokao nchi za Mashariki ya Kati, pamoja na
Bara ya Ulaya na Afrika, kwa kutumia mifumo ile ile iliyowekwa kwa
wagonjwa ya kuambukiza kama Ebola ambayo yaweza kuingia nchini kupitia
mipaka yetu. Ufuatiliaji huu hufanyika bila
kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa wasafiri.
- Kuendelea
na upimaji wa sampuli zinazohisiwa kuwa na ugonjwa huu. Aidha Maabara ya
taifa imejengewa uwezo wa kupima virusi vya Corona virusi. Sampuli
zilizopimwa kuanzia April mpaka Juni 2015 zimethibitisha kuwa hakuna
ugonjwa huo hapa nchini.
- Kutoa
taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa
Mikoa na Wilaya kwa Tanzania bara. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna
mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa
watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli ikiwa ni pamoja na
vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa
huu.
- Kutoa
elimu wa jamii kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na
maeneo ya mipakani kuhusu dalili za ugonjwa huu na jinsi ya kujikinga na
maambukizi ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.
- Kutoa
mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya
maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa
atapatikana huku wakizingatia kanuni za usafi (Infection, Prevention and Control)
- Wizara
inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili kwa
wasafiri watakaokwenda au kurudi katika maeneo tajwa yaliyothibitishwa
kuwa na ugonjwa huu.
Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na
hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa nchini.
Ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia ya
hewa iwapo mgonjwa atokohoa au kupiga chafya bila kujikinga au pia kugusa
sehemu zenye ugonjwa huo na kujigusa mdomomi au puani. Kwa kuzingatia hali
hiyo, wizara inapenda kutoa tahadhari kwa wananchi juu ya umuhimu wa kunawa mikono vizuri kwa sabuni na maji
mara kwa mara na pia kuzuia mdomo na pua kwa kitambaa au karatasi laini (tissue
paper) wakati unapokohoa au kupiga chafya.
Mpaka sasa hakuna kizuizi cha
kusafiri kutoka nchi moja hadi nyingine. Hata hivyo inashauriwa kwamba mtu
yeyote anayesafiri kwenda Mashariki ya Mbali na nchi za Asia afahamu kuwa kuna
hatari ya ugonjwa huu na kwamba anatakiwa atoe taarifa mapema kwenye taasisi za
huduma za afya iwapo ataona dalili kama hizi wakati akiwa safarini au wakati
amewasili toka nchi ambazo zina ugonjwa huu.
Vilevile, wananchi wanashauriwa
kutoa taarifa kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu mara
watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikali – Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
25/06/2015

Post a Comment