Vladimir Putin asema Urusi ina kombora lisiloweza kuzuiwa
Urusi imeunda kombora jipya ambalo haliwezi kutunguliwa na linaweza kufika pahala popote duniani, kwa mujibu wa Rais Vladimir Putin.
Bw Putin amekuwa akieleza sera zake muhimu za muhula wa nne, Taifa hilo linapokaribia kufanya uchaguzi katika siku 17.
Rais huyo anatarajiwa kushinda.
Amesema kombora "halipai juu sana, ni vigumu sana kulitambua likipita, lina uwezo wa kubeba kichwa cha nyuklia na linaweza kufika popote pale. Aidha, njia linayofuata haiwezi kutabirika na adui, linaweza kukwepa vizuizi na kimsingi haliwezi kuzuiwa na mifumo ya sasa ya kinga dhidi ya makombora na hata mifumo inayotarajiwa kuundwa siku zijazo."
Katika nusu ya kwanza ya hotuba hiyo yake kwa taifa, ameahidi kupunguza viwango vya umaskini nchini humo.
Kisha, ameonesha mkusanyiko wa silaha mpya, likiwemo kombora alilosema linaweza "kufika pahala popote duniani".
Hotuba hiyo ya Bw Putin imeendelea kwa saa mbili.
Kiongozi huyo anakabiliwa na wapinzani saba, lakini hakuna mmoja kati ya hao anayetarajiwa kutoa ushindani mkubwa kwake.
Rais huyo hakushiriki katika mdahalo wa wagombea uliooneshwa moja kwa moja kwenye runinga Jumatano na kuwashirikisha wagombea hao wengine.
Kiongozi wa upinzani Alexei Navalny hajakuwa akifanya kampeni.
Amezuiwa kuwania na ametoa wito kwa wapiga kura wanaomuunga mkono kususia uchaguzi huo.
Rais Putin hajafanya kampeni sana na kufikia sasa alikuwa hajazungumzia sana mipango yake ya miaka sita ijayo.
Huku akitumia skrini kubwa, ameonyesha video za alichosema ni kombora jipya la Urusi.
Amesema kombora hilo haliwezi kuzuiwa na mfumo wa kinga ya makombora wa Marekani barani Ulaya na Asia.
Kadhalika, ameonesha video ya ndege isiyo na rubani inayoweza kufanya kazi chini ya bahari.
Kwenye hotuba hiyo yake kwa kikao cha pamoja cha mabunge mawili, amewahamasisha raia kupendekeza majina ya kupewa mifumo hiyo miwili ya silaha.
Ulinzi
Putin amesema uwezo wa kijeshi wa Urusi umepangwa na kustawishwa kwa lengo la kudumisha amani duniani.
Hata hivyo, amesema iwapo mtu yeyote yule atathubutu kurusha silaha za nyuklia dhidi ya Urusi, atajibiwa mara moja.
Operesheni ya kijeshi ya Urusi Syria, ambapo anasaidia Rais wa Syria Bashar al-Assad dhidi ya waasi na amesema hiyo inadhihirisha kuimarika kwa uwezo wa Urusi katika kujilinda.
Amesema pia kwamba daraja la kuunganisha Urusi na rasi ya Crimea litafunguliwa miezi michache ijayo.
Urusi iliteka Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014 wakati wa muhula wa sasa wa Bw Putin.
Kiongoiz huyo amesema Urusi inalinda maslahi yake katika eneo la Arctic kwa kuimarisha miundo mbinu yake ya kijeshi eneo hilo.
CREDIT:BBC SWAHILI
Post a Comment