Wananchi na watumishi pamoja na wale ambao wanafanya kazi sekta binafisi mkoani Geita,wametakiwa kutumia fursa ya chuo kikuu huria ili kuongeza kiwango cha elimu pamoja na maarifa ambayo yatawasaidia kwenye shughuli zao za kila siku.
Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu mstaafu,ambaye ni Mkuu wa chuo kikuu huria nchini,Mizengo Pinda wakati wa ziara yake ya kutembelea na kujionea shughuli ambazo zinafanywa na chuo hicho mkoani humo pamoja na kuzungumza na wanafunzi.
Mh,Pinda alisema ni vyema kwa wakuu wa mikoa kuendelea kuhamasisha watumishi ambao wapo kazini kujiongezea uwezo zaidi kielimu kwenye vyuo vikuu huria ili kufikia adhima ya Tanzania ya viwanda ifikapo 2025.
“Mkuu wa mkoa na katibu tawala tusaidieni sana kuhamasisha kundi la watalaamu ambao wapo serikalini kutumia fursa hii kujiongezea uwezo ili waweze kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kielimu”Alisisitiza Pinda.
Naye mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi alisema suala la elimu halina mwisho kwani pindi unavyozidi kuongeza elimu ndio unafungua mianya ya kukabiliana na janga la umasikini.
“Elimu haina mwisho jinsi ambavyo unachukua nafasi ya kupata elimu unapata uwezo wa kupigana vita vya umasikini vita vya kuondoka kiwango ulichopo kwenda kwenye kiwango cha juu hivyo basi natoa wito kwa wananchi wote waliopo mkoa wa Geita kutumia fursa hii kujiendeleza kielimu kwenye chuo hiki huria”Alisema Luhumbi.
Hata hivyo mkurugenzi wa chuo kikuu huria tawi la Geita,Ally Abdul,ameishukuru serikali kwa kuwapatia hati miliki ya kiwanja kwa ajili ya kuongeza majengo pamoja na msaada wa vitabu 285.
Chuo kikuu huria Tawi la Geita kilianza mwaka 2012 na kufanya kazi rasmi mwaka 2013 kikiwa na takribani wanafunzi 74 na wengi kati ya hao walisajiliwa kutoka Mwanza wakati huo Geita ikiwa ni wilaya idadi ya wanafunzi iliongezeka kwa mwaka 2014 na 2015 kufikia 118 na mwaka huu kuna jumla ya wanafunzi ni 285.
Post a Comment