Mtanzania akamatwa na kilo 32 za dhahabu Kenya
MAMLAKA ya Mapato Kenya (KRA)
imesema, imemkamata raia wa Tanzania akiwa na kilo 32.25 za dhahabu zenye
thamani ya shilingi milioni 100 za nchi hiyo ambazo ni sawa na takribani
shilingi bilioni mbili za Tanzania.
Taarifa ya KRA imesema, mtuhumiwa huyo alikamatwa
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) akiwa na miche ya
dhahabu.
Kwa mujibu wa KRA, Mtanzania huyo mwenye umri wa miaka
46 alikutwa na gramu 32,255.50 za madini hayo na hati ya malipo ya Dola za
Marekani 859,890.
Taarifa ya KRA imeeleza kwa, kijana huyo alifika JKIA
Ijumaa Februari 16 saa 9.05 alasiri kwa ndege ya shirika la Precision, alitoka
Mwanza akapita Kilimanjaro na alikuwa anakwenda Dubai kwa ndege ya Shirika la
Ndege la Kenya, Kenya Airways.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, usafirishaji bidhaa kwa
siri vikiwemo vito vya thamani ni kinyume cha kifungu cha 85 (3) cha Sheria ya
Usimamizi wa Forodha ya mwaka 2004 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Upelelezi kuhuus dhahabu iliyokamatwa unaendelea na
sasa ipo chini ya KRA na mamlaka za usimamizi wa forodha za mipaka.
SOURCE:HABARILEO
Post a Comment