Header Ads

Mwinjilisti Graham afariki dunia akiwa na miaka 99

Mhubiri wa injili Billy Graham, aliyepata umaarufu mkubwa duniani katika karne ya 20 amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 99.
Graham, raia wa Marekani, alieanzia kuhubiri jijini London Uingereza mnamo mwaka 1954, alikusanya maelfu ya watu kila mahali alipofanya mikutano ya hadhara ya injili.
Afrika Mashariki, Graham aliwahi kuhubiri Tanzania, miaka 55 iliyopita, wakati nchi ikiitwa Tanganyika, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Afrika miaka ya 1960. Takriban "watu 40,000 walihudhuria mkutano huo wa siku moja, tarehe Feb 28. 1960", kwa mujibu wa mtandao wa shirika lake.
Kwa zaidi ya miaka 60 inakadiriwa kuwa amehubiri  jumla ya watu milioni 210.
Alikuwa Mkristo akiwa na umri wa miaka 16 baada ya kumsikiliza mhubiri mmoja na kuanza huduma ya mahubiri mwaka 1939.
Graham, ambaye alifanya kazi kama afisa wa mauzo, aliendelea  kuwa mmoja wa wahubiri wenye ushawishi mkubwa miongoni mwa watu wa dini zote huku akiwashauri marais na viongozi wengine wengi duniani juu ya imani ya Kikristo.
Mwaka 1949, alipata umaarufu wakati alipohubiri kwa wiki nane kwenye hema kubwa huko Los Angeles.
Wakati wa harakati za mashirika ya kupigania haki za binadamu, Graham aliibuka kuwa mkosoaji mkubwa wa ubaguzi wa rangi nchini Marekani.
Ni muhubiri aliyeepuka kashfa mbalimbali zilizowazonga wahubiri wengi waliotumia runinga kusambaza injili.
Alijenga uhusiano wa kirafiki na marais kadhaa wa Marekani kuanziaTruman hadi Nixon na hata Obama. Mkutano wake wa mwisho wa hadhara ulikuwa mwaka 2005 jijini New York Marekani akiwa na umri wa miaka 86.
Rais Donald Trump amemuelezea Graham kama "mwanaume wa kipekee".
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Trump amesema "Mhubiri maarufu wa Injili Billy Graham. Hakuna aliyekuwa kama yeye! Atakumbukwa na Wakristo na watu wa dini zote. Mwanamume wa kipekee kabisa."

Bill Graham ni baba mzazi wa Mkurugenzi wa Shirika la Samaritan Purse Franklin Graham wa Marekani. Shirika ambalo liligharamia kukodisha ndege maalumu aina ya DC 8 kupeleka wanafunzi waliojeruhiwa katika ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent Karatu Arusha, mwezi May 2017.

No comments