Naibu waziri wa madini Stanslaus Nyongo amesema kuwa serikali ya awamu ya tano haiko tayari kuona mtu akilalamika ,kunyanyaswa ama kunyimwa haki yake.
Kauli hiyo ameitoa wakati akiongea na wananchi wa kijiji cha Nyakabale kata ya Mgusu Wilayani Geita wakati wa ziara yake ya siku mbili Mkoani humo ya kuzungukia maeneo ya uchimbaji pamoja na kusikiliza kero za wananchi ambao wanazunguka kwenye baadhi ya maeneo ya mgodi wa Geita(GGM).
Hatua hiyo ya Naibu Waziri Nyongo imekuja baada ya kusikia malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya mgodi wa GGM kushindwa kuwalipa fidia kwa muda mrefu pamoja na kuwepo kwa maagizo mengi ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakifika Mkoani humo.
“Tukikaa kwenye viyoyozi hatuambiwi ukweli na wamiliki wa migodi lakini tunapo fika katika eneo husika tunapata ukweli , unakuta mtu kazaliwa hapo kakulia hapo amejenga ana watoto halafu mtu anakuondoa kwa madai kuwa upo kwenye leseni yake hainiingii akilini kama unahitaji eneo langu njoo tukae tumalizane unipe changu mimi nisepe inakuwa nilipe nisepe ”alisema Nyongo.
Hata hivyo aliwataka watu wa mgodi huo kuwalipa wananchi hao ama waondoke wawaachie wananchi hao eneo lao waendelee kuchimba na sio kuwazuia ikiwa hawafanyi shughuli za uchimbaji kwa sasa .
Awali Akitoa malalamiko kwa Naibu waziri mwananchi wa Nyakabale kwa niaba ya wenzake Joseph Kihengu alimwambia Naibu waziri kuwa wanailaumu serikali iliyopita inawezekana wakati wanabinafsisha mgodi huu na wao walibinafsishwa humo bila kujua.
“Mheshimiwa kipindi cha nyuma usingeweza kupata umati kama huu, umati huu umetokana na imani ya serikali ya awamu ya tano waliyo nayo hivyo serikali iwaangalie kwa jicho la tatu ili watu wa Nyakabale wajue hatima ya maeneo ambayo yapo ndani ya bikoni za mgodi wa GGM”Alisema Joseph.
Post a Comment