Kisa cha kwanza cha mwanamume aliyejibadilisha jinsia 'kumnyonyesha mtoto'
Mwanamume aliyejibadilisha jinsi na kuwa mwanamke amefanikiwa kumnyonyesha mtoto katika kisa cha kwanza cha aina yake kuwahi kushuhudiwa, watafiti wanasema.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 30 alitaka kumnyonyesha mtoto baada ya mpenzi wake aliyejifungua kusema hataki kumnyonyesha mtoto huyo, hayo ni kwa mujibu wa jarida la afya la watu waliojibadili jinsi.
Alifanikiwa kunyonyesha baada ya kumeza dawa na kukamua maziwa, ripoti hiyo inasema kutoka nchini Marekani.
Mtaalamu wa Marekani anasema utafiti huo huenda ukachangia visa zaidi vya wanaume waliojibadilisha jinsia kuwa wanawake kunyonyesha watoto.
Mwanamke huyo aliyekuwa anapokea matibabu ya kubadili homoni zake mwilini kwa muda wa miaka 6, lakini hajafanyiwa upasuaji kubadili sehemu zake za siri, wakati alipowaomba madaktari wamsaidie atimize lengo lake la kumnyonyesha mtoto.
Kabla ya mtoto huyo kuzaliwa, madakatari walimpa dawa za miezi mitatu unusu kumsaidia kupata maziwa, kwa kawaida dawa hizo hupewa wanawake waliowaasili watoto au waliojipatia watoto kupitia wanawake wanaobeba mimba kibiashara kuwaisaidia wasioweza kuzaa.
Dawa hizo husisimua homoni mwilini kushinikiza kutoa maziwa na kuzuia homoni za kiume na pia alihitajika kukamua maziwa yake.
Na matokeo yake, yalimsababisha mwanamke huyo kuweza kupata maziwa kiasi.
Watafiti wanasema mtoto huyo alikunywa maziwa hayo tuu kwa wiki zake sita za uhai, wakati ambapo ukuaji wake, ulaji na uendaji haja wake ulikuwa unaendelea kama kawaida.
Baada ya hapo, mtoto alianza kupewa maziwa ya mkebe kwasababu maziwa yalianza kupungua.
Mtoto huyo sasa ana miezi sita na anaendelea kunyonya kama sehemu ya lishe yake, wahariri wa utafiti huo wanasema.
Dkt Channa Jayasena, mhadhiri mkuu katika chuo cha Imperial College anayejishughulisha na masuala ya uzazi amesema, utafiti huo ni 'hatua nzuri'.
Amesema ameshasikia visa kadhaa nchini Uingereza vya wanaume waliogeuka kuwa wanawake wanasaidiwa kunyonyesha, lakini mpaka sasa hakuna ripoti iliyochapishwa.
Amesema:"Tunachohitaji kufanya nikuvikusanya visa hivi na tusaidiane ki mawazo, tutafute mbinu muafaka kuwasaidia kunyonyesha bila ya kuwadhuru kiafya."
Watafiti wanasema haijabainika wazi iwapo dawa zote zinazotumika zinahitajika kufanikisha wazazi hao kuwawezesha kunyonyesha.
Wamesema uchunguzi zaidi unahitajika kubaini matibabu halisi ya wanaume wanaojibadili jinsi kuwa wanawake wanaotaka kunyonyesha.
SOURCE:BBCSWAHILI
Post a Comment