"GGM HAINA TATIZO NA SERIKALI" RC LUHUMBI
Serikali Mkoani Geita,imesema kuwa haina tatizo na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) na kwamba haiwezi kuendelea kukubali jambo baya ambalo linafanywa na mtu mmoja kuchafua sura ya mgodi mzima kwani shughuli ambazo zimeendelea kufanywa zimeendelea kuleta manufaa kwa Taifa na mkoa kwa ujumla.
Akizungumza baada ya ziara yake ya kutembelea na kuona namna ambavyo mgodi huo umekuwa ukifanya shughuli za uzalishaji wa dhahabu,Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi alisema mgodi na serikali ni kitu kimoja kutokana na kwamba wamekuwa wakilipa fedha kwa Taifa pasipo kuwa na udanganyifu wa aina yoyote.
“Hatuwezi tukakubali jambo lolote lile likafanywa na mtu mmoja likaonekana uongozi wa mgodi na serikali kwamba hatuna mahusiano mazuri mimi napinga kwa nguvu zote mgodi na serikali tuko kitu kimoja hawa ni wawekezaji wazuri wanalipa fedha zinazotakiwa kwa wakati na kama kuna changamoto chache chache zinaelezeka tukae pamoja tutatue”Alisema Luhumbi.
Kuhusu miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa na mgodi huo,Luhumbi alisema kuna makosa mengi ambayo yalifanyika kwa miaka ya nyuma kutokana na miradi ambayo ilikuwa ikipangwa wananchi walikuwa hawafahamu na kwamba kutokana na timu ambayo imewekwa kwa sasa ya mgodi wanaamini miradi ambayo imepangwa itatekelezwa kwa haraka na kwa wakati.
“Makosa mengi yalifanyika katika miradi ya nyumba kosa moja ambalo lilifanyika wewe huwezi kupanga mradi bila ya wananchi kuwa tayari wanafahamu huo mradi na kuna maandalizi mazuri lakini kwa timu ambayo imetengenezwa kwa wakati huu wakurugenzi wote wameshakaa na wamepitisha kwenye vikao halali vya halmashauri kwa hiyo hili jambo lipo kisheria sana hapa tulipo kuna hatua moja ambayo imebakia ya kuweka sahihi ili miradi ianze kutekelezwa”alisema Luhumbi.
Aidha Meneja mahusiano wa mgodi huo Tenga B Tenga alisema lengo la mgodi ni kuhakikisha wananchi ambao wanauzunguka wananufaika katika nyanja mbali mbali zikiwemo za afya,uchumi pamoja na Elimu.
Post a Comment