Freeman Mbowe na vigogo wengine wa Chadema waripoti polisi
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho wamekwenda kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana Jumatatu Februari 27, 2018 Mbowe amesema wamekwenda kuripoti kuitikia wito wa Polisi.
Amesema katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji hatakwenda kwa kuwa yupo nje ya nchi na atakaporejea atakwenda kwa kuwa hawana sababu ya kugoma.
Februari 20,2018 Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo Mbowe.
Wito huo ulikuja siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.
Mbowe akizungumza na waandishi wa habari amesema wana taarifa kuwa watakamatwa na kwamba kuna mpango wa kubambikiziwa kesi.
Post a Comment