Tundu Lissu,Abdallah Mtolea Wapinga Azimio la Bunge Kumpongeza Rais Magufuli
Azimio la Bunge la kumpongeza Rais John Magufuli kwa hatua anazochukua kukabiliana na upotevu wa mapato ya serikali katika sekta ya madini jana liligawa Bunge baada ya wabunge wa upinzani kulikataa wakati wenzao wa CCM wakilikubali.
Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu alipowahoji wabunge kama wanakubali azimio hilo, wabunge wote wa CCM waliitikia "ndiyooo" wakati wale wa upinzani walisema "siyooo".
Azimio hilo lenye kurasa mbili liliwasilishwa bungeni jana na Mbunge wa Newala Mjini (CCM), George Mkuchika na baada ya hapo wabunge walipata nafasi ya kulijadili.
“Bunge linamuunga mkono Rais John Magufuli na lipo tayari kutoa ushirikiano wa dhati kadri itakavyohitajika kuhakikisha juhudi hizi hazipotei bure na sekta ya madini inachangia maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla,” alisema Mkuchika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Lakini, aliposimama akiwa wa kwanza kuchangia hoja ya maazimio hayo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alipinga akisema ni kinyume na majukumu ya Bunge hivyo kulitaka lisiendelee na taratibu za kumpongeza Rais akisema alichokifanya si kipya.
“Kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali, siyo kuipongeza au kuiimbia mapambio. Hili siyo azimio la Bunge, bali wana-CCM kumpongeza mwenyekiti wao,” alisema mnadhimu huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Alisema kinachofanywa na Rais Magufuli kilifanywa pia na watangulizi wake waliounda tume kadhaa na kwamba mpaka azimio hilo linajadiliwa, bado usafirishaji wa dhahabu inayochimbwa kwenye migodi mbalimbali nchini unaendelea.
“Dhahabu na madini mengine yanaendelea kusafirishwa hivi sasa. Ripoti za Profesa Mruma na Profesa Osoro ni professorial rubbish. Ni uongo, uongo, uongo,” alisema Lissu.
Ingawa alitakiwa kufuta neno rubbish kwenye mchango wake, Lissu alifafanua kwamba ripoti za wenyeviti hao wa kamati mbili za Rais za kuchunguza makontena 277 ya mchanga wa dhahabu, hazina taarifa sahihi.
Kuhusu azimio hilo kutokuwa na jipya, alisema Rais mstaafu, Benjamin Mkapa aliunda kamati ya Jenerali (Robert) Mboma mwaka 2002, ya Dk (Jonas) Kipokola mwaka 2004 kisha ya Dk (Enos) Bukuku mwaka 2005. Alisema hata Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete naye aliunda mbili za Lawrence Masha na Jaji Mark Bomani.
Alisema kama Bunge linataka kupongeza kuhusiana na kamati zilizoundwa na Rais Magufuli, basi halina budi kuanza na watangulizi hao ambao walifanya kama anachokifanya sasa kwa masilahi ya Taifa huku akipendekeza semina itolewe kwa wabunge ili kuwaongezea uelewa wa masuala ya madini na kuwafanya wachangie wakiwa na ufahamu wa kutosha kuhusu sekta hiyo.
Lissu alipingwa na Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde ambaye alitoa sababu za kumpongeza Rais Magufuli akisema kuna tofauti kati ya kamati alizoziunda na zile za watangulizi wake.
“Rais ameenda mbali zaidi. Ripoti imepokewa hadharani na wananchi wote wameisikia. Hii ni hatua ya mbele. Haiwezekani Taifa lisimpongeze Rais anapofanya mambo yanayoonekana,” alisema.
Alisema ameona clip (video fupi) za mawaziri wakuu wastaafu waliohamia upinzani; Edward Lowassa na Frederick Sumaye wakimpongeza Rais kwa hatua zake.
Lakini, Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea alionekana kuungana na Lissu akiongeza kwamba maazimio hayo hayakuwa sawa kwa maelezo kwamba kilichofanywa na Rais Magufuli mpaka sasa hakijapiga hatua kubwa zaidi ya kilichofanywa na watangulizi wake.
Alisema suala la msingi ni kudhibiti wizi wa rasilimali nchini akikumbusha kwamba Kikwete pia aliunda tume lakini hata baada ya kupelekewa ripoti, hakufanya chochote hatua ambayo Rais Magufuli amefikia mpaka sasa kwenye vita aliyoianzisha.
Alisema hoja ya wizi wa madini ilianzishwa siku nyingi na wabunge ambao walionekana kuwa si wazalendo. “Kama Mkapa na Kikwete tungewapongeza kwa kuunda tume leo ingekuwaje? Bunge tusiwe washangiliaji,” alisema.
Alikumbusha pia kwamba Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba alipiga kelele, Dk Hamis Kigwangallah wa Nzega Vijijini (CCM) aliteswa, Tundu Lissu, Zitto Kabwe wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo) na John Mnyika wa Kibamba (Chadema) walilizungumza suala hilo lakini walibezwa.
Alisema kwa kuwa suala hilo sasa linazungumzwa na mtu anayependwa, linaungwa mkono.
Katika mchango wake, Hasunga ambaye ndiye aliyekuwa mtoa hoja alisema hatua ya Rais kuzuia usafirishaji wa mchanga nje ni muhimu inayopaswa kuungwa mkono na Watanzania wote.
“Jimboni na mkoani kwangu kuna madini mengi, hatustahili kuwa maskini,” alisema.
Akiunga mkono hoja hiyo, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema anachokifanya Rais Magufuli ndicho alichoahidi hata kabla hajashika wadhifa huo,
“Aliahidi watu watalima kwa meno, tunaona mafisadi wakilima kwa meno. Namuomba hata watu wanaowatetea wezi hawa awalimishe kwa meno pia.”
Mbunge huyo ambaye aghalabu huzungumza kwa mbwembwe aliungwa mkono na Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa ambaye alitaka neno uzalendo liondolewe kwenye kamusi ya Kiswahili endapo kuna mtu atapinga yanayofanywa na Rais Magufuli.
“Tunaamini mambo haya yakitekelezwa vyema tutakuwa na barabara za lami na hatutakuwa na deni la Taifa,” alisema Mchengerwa.
Post a Comment