Mwanasheria mkuu TBS ahukumiwa miaka mitano jela au faini ya Milioni 13.9
Baada ya kuachiwa huru siku ya Jumatano na kukamatwa tena, jana aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baptister Bitaho (54) amehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 13.9 au kifungo jela miaka mitano baada ya kusomewa upya mashtaka na kukiri.
Bitaho alifikishwa tena katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana asubuhi na kusomewa mashitaka nane likiwemo la kufanya kazi nchini bila kibali na kutoa taarifa za uongo.
Bitaho ambaye ni Raia wa Burundi, alifutiwa mashtaka yake, na baadae kukamatwa, alisomewa hukumu hiyo, na Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.
Akisoma hukumu hiyo Nongwa alisema kuwa mahakama imesikiliza maombi ya pande zote mbili na kwamba katika kosa la kwanza hadi la saba mshitakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh laki tano au kifungo jela kuanzia miaka miwili hadi mitatu na kwamba kosa la nane mshitakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 10 au kifungo jela miaka mitano.
Alisema, kwa taratibu zilizopo, baada ya mshitakiwa kukutwa na hatia anatakiwa kupelekwa Uhamiaji na kurudishwa nchini kwao ili aombe uraia wa Tanzania upya.
Kabla hukumu hiyo kusomwa, Wakili wa utetezi, Aloyce Komba alidai kuwa mshitakiwa hakuwahi kuvunja sheria ya kijinai kwani alikuwa mwaminifu na hakuwahi kutoa siri ya nchi licha ya ukimbizi wake.
Komba pia aliongeza kuwa, tangu mteja wake apate kashfa hiyo, ameathirika kiuchumi kwa kuwa alitakiwa kustaafu miaka sita ijayo lakini sasa anakosa mapato yake.
‘’Naomba mahakama isitoe adhabu kubwa kwa mteja wangu kwani pamoja na ukimbizi wake, kutokana na vita za mara kwa mara zinazotokea nchini Burundi, mshitakiwa ameanzisha kituo cha kulelea watoto yatima wa Tanzania na Burundi hivyo amekuwa na msaada,’’alidai Komba.
Akimsomea maelezo ya awali (PH), baada ya kukiri mashtaka yake, Mwendesha Mashitaka wa Uhamiaji, Method Kagoma alidai wazazi wa Bitaho waliingia nchini mwaka 1958 na kisha kurudi tena mwaka 1972 huku yeye Bitaho akiwa mtoto mdogo.
Aliidai baada ya kukua, mshitakiwa huyo alijiunga na elimu ya msingi, sekondari na vyuo hapa nchini na kwamba mwaka 2001 aliajiriwa na TBS kama mwanasheria.
Katika mashitaka yake inadaiwa Mei 19, mwaka huu maeneo ya Ofisi ya Uhamiaji iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwa mkimbizi na Raia wa Burundi, alitoa taarifa za uongo kwa ofisa wa uhamiaji.
Alidaiwa kuwa alijitambulisha kuwa ni raia wa Tanzania na kuonesha Kitambulisho cha Taifa chenye jina lake ambacho alikipata kinyume na sheria huku akijua kwamba anajiongezea kosa.
Kagoma alidai, Oktoba 19, 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wilayani Ilala Dar es Salaam, akiwa mkimbizi na Raia wa Burundi, alishindwa kutimiza masharti yaliyotolewa Septemba 11, 2013 na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji ambapo alishindwa kurejesha hati ya kusafiria aliyoipata isivyohalali.
Imeendelea kudaiwa kuwa, Juni 22, 2011 katika Ofisi za Uhamiaji za Mkoa, alitoa taarifa za uongo katika fomu ya kuombea hati ya kusafiria CT5 (Ai) yenye namba 05381440 kwa lengo la kupata hati hiyo.
Aidha mshtakiwa Bitaho anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa kutoa kiapo kuonesha kuwa baba yake ni raia wa Tanzania kitu ambacho sio kweli na kwamba alitoa barua kutoka Ofisi ya Kata ya Yombo Vituka iliyomtambulisha kuwa ni Mtanzania kwa lengo la kupata hati ya kusafiria.
Mshitakiwa Bitaho alitoa pia barua ya kuajiriwa aliyoambatanisha na fomu ya maombi ya hati ya kusafiria kuonesha ni Mtanzania kitu ambacho alijua si kweli.
Aidha anadaiwa kujipatia kadi ya kupigia kura kinyume na sheria na kwamba Mei 19 na pia amejihusisha na kazi kama Mwanasheria Mkuu wa TBS bila kuwa na kibali.
Post a Comment