Kamisha Siang’a asema wauza ‘Unga’ walijaribu kumuua wiki iliyopita......Asimulia Wanavyoishi Kifahari Gerezani
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Siang’a amesema kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya walitaka kumuua wiki iliyopita.
Kamishna Siang’a ameeleza hayo katika mahojiano maalum aliyofanya na gazeti la Mwananchi kuhusu maendeleo ya vita dhidi ya biashara hiyo haramu, ikiwa ni takribani miezi mitano tangu ateuliwa kuongoza kitengo hicho nyeti.
“Wiki iliyopita tu hapa [wauza dawa za kulevya] walitaka kuniua,” alisema Siang’a ingawa hakueleza kwa kina kuhusu jaribio hilo baya dhidi yake. “Wanaofanya biashara hii wana uwezo wa kufanya chochote wanachotaka. Kabla jamii haijatuhukumu ni vyema ikatambua kuwa tuna changamoto kubwa,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Kamishna Siang’a alisema kuwa wanaofanya biashara hii haramu ni watu wakubwa ambao hufadhili kazi za Serikali, viongozi wanaowalina na madhehebu mbalimbali ya dini.
Alisema kuwa yupo mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya ambaye alikuwa akionekana kama mtu mwema sana kwenye jamii, akifadhili taasisi moja ya Serikali pamoja na kuwasomesha watoto wa vigogo na kufadhili shughuli zao za harusi, lakini ameshakamatwa na anatumikia kifungo cha maisha jela.
Hata hivyo, Siang’a alisema kuwa wamepata taarifa kuwa mfanyabiashara huyo anaishi maisha ya kifalme gerezani na kwamba huenda hata usiku halali ndani ya gereza hilo.
“Tunapata taarifa kuwa anahudumiwa vizuri gerezani, na inavyosemekana kuwa huenda halali hata huko. Anachukuliwa usiku na kupelekwa kwake kulala, asubuhi anarudishwa,” alisema.
Alitoa mfano mwingine wa nguli wa dawa za kulevya aliyefungwa gerezani, kuwa kabla ya kuingia alikarabati gereza na kukodisha nyumba za jirani kwa ajili ya kuweka watu ambao watakuwa wanampikia vyakula, hivyo ameendelea kuwa na afya nzuri akiwa gerezani.
Alisema hayo yote hufanyika kwa ushirikiano wa baadhi ya askari wa gerezani na wakuu wa gereza husika.
Kamishna Siang’a alisema kuwa Mamlaka hiyo hairudishwi nyuma na kwamba hadi sasa wameshawakamata vinara 15 wa dawa za kulevya ambao amewataja kama watu wenye jeuri ya pesa.
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment