Header Ads

Mtawa Katoliki aburuzwa kortini kwa wizi


KANISA Katoliki Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, limemfikisha mahakamani mtawa wa kanisa hilo, Emmanuela Nindi (40) kwa tuhuma ya kuliibia Sh milioni 28.8.
Mtawa huyo ambaye alikuwa ni Mhasibu wa jimbo hilo, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya hiyo ili ajibu tuhuma hiyo inayomkabili mbele yake.
Ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Seif Kilugwe mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbinga, Magdalena Ntandu kwamba mshtakiwa huyo anadaiwa kufanya kosa hilo katika kipindi cha mwaka jana.
Inspekta Kilugwe alidai kuwa baada ya kutenda kosa hilo, mtawa Emmanuel alikimbia na kutokomea kusikojulikana, ndipo uongozi wa jimbo ulipofanya jitihada ya kumtafuta na baadaye ulimpata na hatimaye kumfungulia mashtaka hayo.
Pia alidai mahakamani hapo kuwa mtawa huyo alikuwa akiiba fedha hizo kidogo kidogo kwa nyakati tofauti hadi zilipofikia kiasi hicho, ambazo zilikuwa zinatokana na miradi ya jimbo pamoja na michango mbalimbali ya waumini wa Kanisa Katoliki.
Hata hivyo, mshtakiwa alipoulizwa mahakamani hapo juu ya kosa hilo analodaiwa kulifanya, alikana mashtaka hayo na kwamba alirudishwa mahabusu kutokana na kukosa wadhamini wawili wenye sifa ya kumdhamini ambapo shauri hilo litatajwa tena Machi 28, mwaka huu.

No comments