Header Ads

Mwanza: RC John Mongella akumbana na vilio vya njaa Sumve

Wakazi zaidi ya 300 wa Kata ya Mwagi wakiongozwa na mbunge wao wa Sumve, Richard Ndassa wamepokea msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kwa mabua ya mahindi mikononi mwao, kuashiria namna zao hilo lilivyoathiriwa na ukame.

Mongella ambaye alikuwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, wakati wa ziara yake kukagua maendeleo ya kilimo wilayani hapa, alikutana na hali hiyo katika Kijiji cha Mwabilanda wakati akitokea Kijiji cha Manawa kukagua mashamba ya pamba.

Wakazi hao walisema wametekeleza wajibu wao, lakini ukame umevuruga malengo yao huku wakiomba msaada wapelekewe chakula haraka.

Awali, akiwa Kijiji cha Manawa wakazi wake walisimama barabarani kwa lengo la kutaka wapatiwe ufumbuzi wa namna Serikali ilivyojipanga kuwanusuru na njaa iliyosababishwa na ukame.

 “Kwa kweli hali yetu ya chakula hapa kijijini ni mbaya. Mimi na umri wangu sijawahi kushuhudia hali kama hii kwa zaidi ya miaka 40,”alisema mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Joseph Nkonoki.

 Alifafanua kuwa baadhi ya wanaume wameanza kutelekeza familia zao kutokana na kukosa namna ya kupata fedha kwa ajili ya kununua chakula.

Akijibu malalamiko hayo Mongella alisema: “Timu ya mkoa itakutana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya wiki ijayo ili kuandaa taarifa ambayo baadaye Serikali itaifanyia kazi.Matokeo yake mtayaona muda siyo mrefu.” 

Mongella aliwashauri wakazi hao kulima mazao yanayostahimili ukame katika kipindi hiki ambacho mvua zimekuwa za kusuasua.

Aliwataka kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kujipanga, huku akisema ukame unachangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

 Pia, Mongella alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo, Mtemi Simeon kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wananchi watakaobainika kukata miti bila kibali chake.

No comments