Rais Magufuli Atoboa Siri ya Kula Christmass Mkoani Singida
Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania,Dk.John Pombe Magufuli,amefichua siri ya kusali Krismasi kwenye kanisa la Parokia ya Moyo wa Yesu, mjini Singida mwaka huu.
Ametaja siri hiyo kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, aliwahi kusali kwenye kanisa hilo na wakati akitoka, alikutana na sista mmoja (hamkumbuki jina) ambaye alimzawadia rozali, na kumwahidi kuwa itamsadia kushinda uchaguzi huo.
Rais Magufuli ametoa siri hiyo jana wakati akizungumza kwenye sherehe ya Krismasi iliyofanyika kwenye kanisa la Porokia ya Moyo wa Yesu, na kuhudhuriwa pia na mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli.
Akifafanua, alisema kuwa rozali hiyo amezunguka nayo kwenye kampeni yake, na mwisho wa siku, alifanikiwa kupata kura za kutosha na hivyo kuwa mshindi.
“Hiyo ndio sababu kubwa au siri ya mimi kufika mjini Singida, na kuungana na wakazi wa mkoa wa Singida na Watanzania kwa ujumla, kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu kristo,” alisema na kusababisha mamia ya waumini kushangilia kwa nguvu.
Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania wote kutumia sikukuu hii ya Krismasi kuimarisha upendo, kuvumiliana na wala wasibaguane ,na kwa njia hiyo,Tanzania itaendelea kupaa kimaendeleo.
Katika hatua nyingine, alisema kuwa Watanzania na hususani wakulima, wahakikishe wanazitumia vizuri mvua zinazonyesha kwa sasa nchini kwa kuchapa kazi ya kilimo kwa nguvu zote na kulima mazao yanayostahimili ukame.
“Ndugu zangu waumini na Watanzania kwa ujumla, acheni kulialia kuwa fedha zimepotea … fedha hazijapotea isipokuwa ninyi wenyewe hamfanyi kazi. Vitabu vyote vya madhehebu ya dini vinasisitiza wajibu wa kuchapa kazi … na vinasema asiyefanya kazi na asile,” alisisitiza.
Akiijengea nguvu hoja yake ya hapa ni kazi tu, alisema kuwa Yesu kristo amezaliwa na fundi mchapa kazi kweli kweli seremala, na hivyo tunaposherehekea Krismasi Watanzania wote wenye uwezo wa kufanya kazi, wafanye kazi huku wakijua hakuna cha bure.
Aidha, Rais Magufuli, aliwataka wakazi wa mkoa wa Singida, kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti, ili kukiwezesha kiwanda kikubwa cha kukamua mafuta ya alizeti cha Mount Meru kupata mbegu za kikudhi mahitaji ya kiwanda.
Awali askofu wa kanisa katoliki jimbo la Singida, Edward Mapunda, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wakazi wa mkoa wa Singida, kutunza mazingira, ili yaweze kuwatunza na wao.
Alisema hivi sasa hali ni mbaya kutokana na binadamu kuongeza kasi ya kuharibu mazingira, kitendo kinachochangia madhara mengi ikiwemo uhaba wa mvua.
“Mimi nashangaa sana, watu wanaendelea kuzaa huku wakiendelea kuharibu mazingira na kutishia nchi kuwa jangwa. Tuna zaa watoto waje wateseke kutokana na uharibifu wa mazingira. Kama tunaendelea kuharibu mazingira, ni vema tuache kuzaa”, alisema Mapunda.
Post a Comment