HUMPHREY Polepole "Bado Naamini Muundo wa Serikali Tatu".
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, amekubali madaraka ya usemaji wa chama hicho, huku aking’ang’ania msimamo wake wa Muungano wa Serikali Tatu, unaopingana na matakwa ya chama hicho.
Polepole alitoa msimamo huo jana kwenye ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari mbele ya mtangulizi wake, Nape Nnauye aliyeonekana kutoridhishwa sana na majibu hayo.
Hata hivyo, Nape alipotakiwa kumzungumzia mrithi wake, alimsifu akisema hana shaka na uadilifu, uzalendo, uwezo, usasa na ujana wake na kwamba huenda ndiyo miongoni mwa sifa zilizochangia uteuzi wake.
Ukweli daima
Akijibu maswali ya waandishi wa habari wakati akitambulishwa na kukabidhiwa ofisi na Nape, Polepole alisema msimamo wake kuhusu kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi kwenye mchakato wa Katiba Mpya uko palepale, akisisitiza, “nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.”
Huku akizungumza kwa umakini na kujiamini, Polepole ambaye alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji mstaafu Joseph Warioba, alisema kwa kuwa aliamini maoni ya wananchi kwenye Rasimu ya Tume ambayo yaliondolewa kwenye Katiba Inayopendekezwa, ataendelea kuamini hivyo na kusisitiza kuwa yeye si mtu wa kubadili maneno.
Miongoni mwa misimamo ya kada huyo wa CCM kuhusu mchakato huo, ni pamoja na kutaka muundo wa Muungano wa Serikali Tatu badala ya mbili, Rais kutoteua wabunge, sifa za elimu kwa wabunge, nafasi za makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu kuwekwa kikatiba pamoja na haki ya kutokuwa mtumwa, uhuru wa habari na vyombo vya habari na haki mbalimbali.
Kuhusu serikali tatu, Polepole aliwahi kukaririwa akisema: “Mpango wa CCM kuingiza ajenda ya serikali mbili ndani ya rasimu ya Katiba, utaiingiza nchi kwenye matatizo. Hii ni kwa sababu, serikali mbili ndani ya Muungano hazitekelezeki.”
Mambo hayo yote pamoja na mengine yaliyowahi kunukuliwa na kada huyo, yaliondolewa kwenye Katiba Inayopendekezwa, ambayo mchakato wake wa kuipigia kura ya ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’, ulisimama tangu Aprili mwaka jana, kupisha Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, Novemba 4 alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Rais John Magufuli alisema hakuwahi kuzungumzia Katiba wakati wa kampeni zake, kwa hiyo si kipaumbele chake na kwamba anachotaka kwanza ni “kunyoosha nchi”, jambo lililoashiria kuwa mchakato umesimama kwa muda usiojulikana.
Katika swali hilo, Polepole aliulizwa kama ataendelea na msimamo wake wa kuamini muundo wa Serikali Tatu; Serikali ya Tanganyika, Zanzibar na Muungano; huku msimamo wa CCM na uliomo kwenye Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na wabunge wa chama hicho, ikitaja mfumo uliopo sasa wa serikali mbili.
“Mimi ni mwanachama wa CCM kwa imani na ninaziishi ahadi za chama na mojawapo ni kusema kweli daima na fitina kwangu ni mwiko.
“Msimamo wangu ni madhubuti kwenye chama changu na Taifa langu. Iliyo haki nitasimamia haki, iliyo kweli nitaisema kweli wakati wote na huwa sibadilishi maneno, ahsante sana,” alisema Polepole.
Kabla ya kueleza msimamo wake huo, Polepole alibanwa kwa swali lingine lililomtaka aeleze msimamo wake kuhusu mchakato huo; kwamba uendelee ulipoishia au urejeshwe kwa maoni ya wananchi yaliyofutwa.
“Sidhani kama kuna mkwamo. Mchakato huu umeahirishwa kwa mazingira ambayo yalikuwa wazi, hata Rais Magufuli ameshalisemea hili, sasa Rais anatunyooshea kwanza nchi kupata utamu wa yale tunayotaka. Wakati ukifika usiwe na shaka, jambo hili lipo kwenye mikono salama chini ya Rais Magufuli,” alisema.
Maridhiano
Alisema mchakato wa Katiba ni muhimu kwa Taifa na unahitaji mwafaka, maridhiano na uelewa, hatua iliyoonekana kuachwa wakati Katiba Inayopendekezwa ilipopitishwa kwa kura.
“Rais ana mwaka mmoja madarakani, anapanga nchi na chama…nafikiri mabadiliko ndani ya CCM na ukitazama kwa sura kubwa misingi ya uadilifu, miiko ya uongozi, uwajibikaji na huduma bora vinavyosimamiwa sasa, utaona dhamira ya Serikali ya CCM kuelekea huko (kupata Katiba),” alisema.
Polepole pia aligusia misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho, huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii, ili CCM ipate wanachama wengi zaidi.
“Tutataka kufundisha wananchi na watu wenye mapenzi mema kuhusu misingi ya chama chetu na hasa imani yake. Kama sisi wanachama wa CCM tukiiishi misingi ya chama hata kwa asilimia 60, hii nchi haitachukua muda mrefu kufika tunakotaka,” alisema.
Kukosoana
Alisema lazima CCM ishughulike na shida za watu na mtaji wake uwe ni wanachama na Watanzania, “tufanye siasa za maendeleo na tupunguze siasa za madaraka… kukosoana ni sehemu ya msingi.”
Awali, Nape ambaye alionekana kukunja uso wakati Polepole akielezea msimamo wake, aliishukuru CCM kwa kumwamini na kumpa nafasi ya uongozi kwa miaka mitano, huku akimmwagia sifa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
“Kama kuna kitu nitakikosa CCM ni kufanya kazi na Kinana. Amenitengeneza kufika hapa nilipo leo. Amekijenga chama na kunilea. Wakati naingia hali ya chama ilikuwa ngumu kidogo, ila kwa ushirikiano wake na wanachama wenzangu tumefika tulipofika.
Siri
“CCM ni zaidi ya shule. Nafikiria baada ya kustaafu nafasi hii, nitaandika kitabu cha kueleza ukatibu uenezi wangu ulivyokuwa. Yapo mambo mengi sijayasema na hayajasemwa na mtu yeyote, nitayazungumza kwa faida ya wengine,” alisema Nape.
Pia alitumia nafasi hiyo kuomba radhi aliowakosea, wakiwamo viongozi wa vyama vya upinzani nchini.
“Watani zangu tumetupiana maneno na vijembe, lakini nia ilikuwa njema kuijenga Tanzania yenye siasa nzuri, ushindani na hoja. Katika hali ile tumekanyagana hapa na pale, binafsi nimewasamehe lakini nao naamini wamenisamehe nilipowaumiza, haikuwa nia yangu,” alisema Nape.
Akimzungumzia Polepole, Nape alisema: “Sina shaka na uadilifu, uzalendo, uwezo, usasa na ujana wake. Nadhani hizo ni miongoni mwa sifa zilizowafanya wale walioamua kumteua kuchukua nafasi hii. Anatosha.”
Post a Comment