MTENDAJI MKUU TEMESA AWATAKA WATENDAJI WAKE KUWEKA MAZINGIRA YA KUJITEGEMEA KWA KUZALISHA MAPATO ZAIDI.
Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (kulia) akisikiliza taarifa ya Meneja wa TEMESA Geita Mhandisi Gilly Chacha (Kushoto) alipotembelea kituoni hapo
Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu akikagua sehemu ya kutengenezea magari katika karakana ya TEMESA Geita alipotembelea kituoni hapo.
Watumishi wa karakana ya TEMESA Geita wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (hayupo pichani) alipotembelea kituoni hapo.
Na Theresia Mwami TEMESA Geita.Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu amewataka watendaji wake katika vituo vyote vya TEMESA nchini kuanza kujenga mazingira ya kujitegemea na kuondokana na fikra za kutegemea fedha kutoka Serikalini.Agizo hilo limetolewa na Mtendaji huyo alipotembelea karakana ya TEMESA iliyopo mkoani Geita na kujionea kazi zinazofanywa na karakana hiyo na kuagiza watendaji wake kutafuta mbinu mbadala ya kuzalisha mapato ili waweze kujiendesha wenyewe.“Naomba muanze mikakati ya kufanya kazi kwa kasi na ubora na kuongeza ubunifu ili kuhakikisha kituo kinakusanya mapato ya kutosha kuweza kujiendesha kwa kuwa serikali hapo baadae haitaendelea kutoa ruzuku kwa taasisi zake zote zinazozalisha” alisisitiza Dkt. Mgwatu.Mtendaji Mkuu huyo amemuagiza Meneja wa TEMESA Geita kuhakikisha anafanya matengenezo sehemu ya kutengenezea magari iliyopo kituoni hapo, kuwapa mikataba watumishi wote wasio na ajira za kudumu, kuhakikisha watumishi wanapata vitendea kazi kulingana na mahitaji ya kada zao, kufuatilia kwa karibu wadaiwa sugu wa kituo, na kuhakikisha madeni yaliyopo sasa yanalipwa pamoja na kuongeza uzalishaji wa kituo hicho.Kwa upande wake Meneja wa TEMESA Mkoa wa Geita Mhandisi Gilly Chacha ameeleza changamoto zilizopo kuwa ni uchakavu wa karakana na vifaa vya kazi pamoja na uwepo wa madeni sugu wanazozidai Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Mbongwe pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Mji wa Geita.“Mtendaji tunakuahidi kuanza kutekeleza agizo lako la kuzalisha mapato zaidi ili tujitegemee na kutotegemea ruzuku kutoka Serikalini kwa kuwa wabunifu na kujituma katika kazi na kukusanya madeni yote tunayodai” alisema Mhandisi Gilly Chacha.Aidha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu amemtaka Meneja wa TEMESA Geita kumpatia taarifa za ufuatiliaji wa madeni ya wadaiwa sugu na taarifa ya mapato yaliyokusanywa na kituo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ili kujua pato halisi la kituo.Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu yupo katika ziara ya kikazi Kanda ya Ziwa na atatembelea vituo vya TEMESA vilivyopo ili kubaini changamoto na kujionea utendaji kazi wa vituo hivyo na sasa yupo Mkoani Geita.
Post a Comment