Header Ads

MIEZI SITA JELA KWA KUTAKA KUJIUA.

MAHAKAMA ya wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemhukumu kijana kutumikia adhabu ya kifungo cha miezi sita gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kujiua mwenyewe.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Ajali Milanzi alisema Mahakama imemuona mshitakiwa Luhende Manangu ana hatia kwa kuwa amekiri mwenyewe kosa lake ,hivyo atakwenda jela miezi sita ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Alisema kitendo cha kujichukulia sheria mkononi ni kosa kisheria hivyo kila mtu ana wajibu wa kufuata sheria za nchi na sio kujiamulia mambo yao.
Kabla mtu hajafanya chochote cha kujidhuru lazima atafakari kabla ya kuchukua hatua.
Awali kabla ya Mahakama kutoa hukumu, Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi wilaya ya Igunga, Elimajid Kweyamba alidai kuwa Septemba 4 mwaka huu, saa 4:00 asubuhi, mshitakiwa Manangu (35) mkazi wa kijiji cha Migongwa kata ya Igurubi, alijaribu kujiua kwa kujichoma kisu mwilini mwake.
Manangu alitenda kosa hilo kinyume na kifungu 217 na 35 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 inayozuia kutenda makosa kama hayo.
Baada ya mshitakiwa kusomewa mashtaka alikiri mbele ya Mahakama kutenda kosa hilo la kujaribu kujiua.

No comments