Felix Joseph akielezea kuchukizwa na namna ambavyo walinzi na wauguzi katika hospitali hiyo wamekuwa na majibu mabaya kwa watu wanaokuja kuwasalimia ndugu zao na wagonjwa pia hali ambayo imekuwa ikiwanyima amani wagonjwa na wale ambao wanakuwa wakiwauguza hosptalini hapo.
Familia yagoma kuchukua mwili wa marehemu wa mzazi wao (maiti) kwa kile kinachodaiwa wauguzi wa hospitali teule ya rufaa ya mkoa wa Geita kuwa na majibu machafu kwa wagonjwa.
Akizungumza na mtandao huu katika mazingira ya hospitali hiyo mmoja kati ya wanafamilia ambae amefiwa na baba yake mzazi,Bahati Chihula mkazi wa kijiji cha Kishinda kata ya Kamhanga wilayani Geita.
Amesema kuwa walimpeleka Baba yao siku ya jumatano ya tarehe 5 mwezi huu kwa lengo la kupatiwa matibabu ya tezi dume lakini jambo la kusikitisha alikutana na huduma zisizostahili za wauguzi hali ambayo imepelekea mzazi wake kupoteza maisha kutokana na kukosa huduma nzuri za afya.
“Tulifukuzwa katika wodi ya wagonjwa kwa madai kuwa hatutakiwi kukaa katika wodi hiyo na tulipotoka nje baada ya dakika chache niliporudi sikumkuta mgonjwa wangu pale wodini na baada ya kuchunguza tukamkuta yupo chooni akigaa gaa na nilipouliza kwanini mgonjwa wangu yupo chooni katika hali ile muuguzi alinijibu wewe hutakiwi kujua nenda zako. Na kutokana na huduma mbovu za hospitali hii imepelekea kuondoa uhai wa baba yangu kwani hakuwa mahututi sana na sisi kama familia hatutachukua maiti mpaka sheria ifuate mkondo wake”Alisema Bahati.
Hata hivyo mmoja kati ya wananchi ambae ana mgonjwa anaye muuguza katika hospitali hiyo Felix Joseph ameeleza tatizo kubwa ni walinzi pamoja na wauguzi kwani wamekuwa wakiwatusi wagonjwa na wananchi wanaokuwa wakifika katika hosptali hiyo.
Kutokana na uzito wa swala hilo mbunge wa Geita vijijini Joseph Msukuma amefikisha malalamiko hayo katika kikao cha sita cha kamati ya ushauri ya mkoa kutaka kujua utawala bora ukoje katika hospitali hiyo na juu ya hatua zilizochukuliwa na mganga mkuu wa mkoa dhidi ya mgonjwa aliyefia chooni .
“Mwenyekiti nilikuwa nataka kuuliza kuhusiana na utawala bora kwenye hospitali ya Mkoa Jana mpiga kura wangu alimleta baba yake mzazi hospitalini hapo cha kusikitisha ni kwamba alifukuzwa na kutolewa nje, je ni haki? naomba mganga mkuu atujibu ameshachukua maamuzi gani juu ya wale ambao wameshiriki katika kitendo hicho cha unyanyasaji”aliuliza Msukuma.
Akijibu kuhusiana na tuhuma hizo za kumwacha mgonjwa na mwisho akapoteza uhai wake, mganga mkuu wa mkoa Joseph Kasala,amefafanua kuwa walipewa mgonjwa huyo akiwa anasumbuliwa na tezi dume na kwamba wakati daktari ambae alitakiwa kumfanyia upasuaji alishindwa kutokana na maumivu aliyokuwa nayo mgonjwa.
Sanjari na hayo mkuu wa mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstafu Ezekiel Kyunga amemwagiza mganga mkuu kwenda hospitalini hapo na kupata habari za kina na kujua ni nani ambae amefanya uzembe wa namna hiyo na kama mtu akibainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
|
Post a Comment