Polisi Wamhoji Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob
Maofisa wa Polisi wamemhoji Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob kabla ya hajakutana na waandishi wa habari kwa madai kuwa wamepata taarifa mkutano wake huo ulilenga kumkashifu Rais John Magufuli.
Maofisa hao waliovalia kiraia walionana na Jacob ofisini kwake na walimruhusu kuendelea na mkutano huo baada ya meya huyo kuwahakikishia kwamba hana nia hiyo bali alitaka kutoa ufafanuzi wa baadhi ya masuala baada ya ujio wa Rais, Kinondoni Jumanne iliyopita.
“Kwa mara ya kwanza meya anahojiwa, lakini niliwaambia wana usalama lengo langu ni nini na sipo kwa ajili ya kumkashifu Rais, ila nafahamu vita iliyopo kati yetu na baadhi ya viongozi,” alisema Jacob.
Pamoja na ufafanuzi huo, Jacob aliwataka baadhi yao (askari) kushiriki kwenye mkutano huo wa wanahabari kufuatilia alichotaka kuwaeleza wanahabari na polisi mmoja alibaki kusikiliza bila kutambulishwa.
Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda alisema hakukuwa na tatizo lolote polisi kuwapo eneo hilo, kwani wanafanya shughuli zao za ulinzi na usalama wa raia na hasa ikizingatiwa kuwa kuna Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Katika mkutano huo, meya Jacob alitoa ufafanuzi wa yaliyojiri Jumanne iliyopita wakati Rais Magufuli alipofanya ziara katika manispaa hiyo na kubatilisha umiliki wa eneo la Magomeni Kota lililokuwa mali ya halmashauri kuwa ya Serikali Kuu.
Meya Jacob aliwaambia wanahabari kuwa uamuzi wa Serikali kuchukua eneo hilo umeisababishia halmashauri yake hasara ya zaidi Sh4.5 bilioni kutokana na gharama walizoingia.
Katika eneo hilo, nyumba 644 zilivunjwa mwaka 2011 kwa miadi ya kwamba zikijengwa upya, wananchi waliokuwa wakiishi hapo wakiwa wapangaji wangerejeshwa, lakini mradi huo ulichelewa kuanza.
Akiwa ameambatana na baadhi ya madiwani, Jacob alisema hasara hiyo imetokana na halmashauri kutumia Sh2 bilioni kumlipa mkandarasi kwa ajili ya michoro ya eneo litakavyokuwa.
Alisema pia manispaa hiyo imetoa Sh1 bilioni kwa mkandarasi Gulf kwa ajili ya kuchora ramani ya ofisi mpya za halmashauri na kusimamia ujenzi wa mradi huo na kutumia Sh700 milioni kuwalipia kodi wapangaji hao baada ya kuwahamisha.
“Faida tuliyoipata ni kwamba wananchi tuliopanga kuwahudumia tayari Rais amewahudumia. Hatupingi maamuzi ya Serikali, lakini wananchi watambue kwamba manispaa haina chochote itakachokipata, bali kila kitu kitakuwa kinafanywa na Serikali Kuu,” alisema Jacob.
Meya alisisitiza kuwa madiwani wa Ukawa hawapingi uamuzi huo ila baadhi ya viongozi wanaomzunguka Rais hawamwambii ukweli wa mambo kuhusu mradi wa Magomeni Kota na kwamba baadhi ya watumishi wa Serikali ndiyo waliosababisha kufikia hatua hiyo.
“Siku ile ningepata nafasi hata dakika tatu, ningemweleza Rais Magufuli ukweli wa mambo wa mradi huu. Lakini kuna baadhi ya viongozi waliomzunguka waliamua kuninyima nafasi hiyo. "
Hata hivyo, Jacob alimwomba Rais Magufuli kukutana naye ili amweleze kwa undani jambo linalomuumiza kuhusiana na masuala ya ardhi yanayoikumbuka Kinondoni.
Alifafanua kwamba, Serikali iliyopita na manispaa hiyo ilishaingia mkataba na kampuni ya Blue Marine ya Romania kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Magomeni Kota ambao ulifikia katika hatua nzuri lakini baadhi ya watumishi wa Serikali waliamua kuweka ‘kauzibe’ na kuipa sifa mbaya Kinondoni.
“Tulikuwa tunasubiri utiaji wa saini kutoka Serikali Kuu, lakini baada ya kuona Kinondoni inaongozwa na Ukawa wameamua kuleta ‘figisufigisu’ za kuukwamisha,” alisema Jacob.
Katika ziara hiyo, Rais Magufuli alielezea kusikitishwa kwake na namna tatizo la wakazi hao lilivyoshughulikiwa na kuwaahidi kuwa Serikali yake itahakikisha hawasumbuliwi.
Post a Comment