Header Ads

Marufuku siasa nyumba za ibada

Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe ameliambia Bunge kuwa mtu akihubiri siasa ndani ya nyumba za ibada anapaswa kuhesabiwa kuwa ametenda kosa.
Amesema kinachoweza kumshtaki mtu ni pale waliokuwapo watakapobainisha kilichofanyika mahali hapo ni kosa na kutaka kutafuta haki.
Dk Mwakyembe ametoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Gando, Othman Omar Haji (CUF) aliyehoji kama kiongozi mkubwa serikalini atatoa kauli za siasa ndani ya nyumba za ibada nini kifanyike.
Katika swali lake la msingi, Haji ametaka kujua ni kifungu gani cha Katiba au Sheria ya Jamhuri ya Muungano kinachofafanua kuhusu kuepuka siasa katika nyumba za ibada na kuchanganya dini na siasa katika mikutano.
Dk Mwakyembe amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza katika utangulizi wake kuwa Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasi, ujamaa na isiyo na dini.
Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 inaeleza bayana katika kifungu cha 9 (2) kuwa chama cha siasa hakitastahili kusajiliwa endapo katiba yake au sera zake zina mwelekeo wa kuendeleza masilahi ya imani ya kidini na kundi la kidini,” amesema Dk Mwakyembe.
Kwa mujibu wa waziri huyo Ibara ya 19 (1) na (3) zinaeleza kuwa kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.
CHANZO:MWANANCHI

No comments