Header Ads

Magufuli acharuka, aitaka Bodi ya Pamba ihame mara moja

RAIS John Magufuli ameiagiza Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kuhamia katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuondoka Dar es Salaam, kwa sababu huko ndiko ambako wakulima wengi wa zao hilo wanapatikana.

Aidha, ameionya bodi hiyo kwamba hataki kusikia kwamba imetoa tena mbegu zisizoota kwa wakulima, na endapo hilo litatokea, atawatumbua viongozi wake.

Rais Magufuli aliyasema hayo mjini Geita wakati akizungumza na wananchi, akiendelea na ziara zake katika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita, ambayo aliianza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Alisema inashangaza kuona kuwa Bodi ya Pamba iko Dar es Salaam wakati wakulima wengi wa zao la pamba wanapatikana katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Geita, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu na Kagera, hivyo kuwataka wahamie katika mikoa hiyo na kuwa karibu na wakulima hao.

Akiwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga, alimtaka aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli kurejea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa huko aliko (katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amepotea njia na kuna mafisadi.

“Wana-Kahama tambueni kuwa Lembeli ni rafiki yangu wa siku nyingi na kuwepo kwake hapa ninategemea mabadiliko makubwa kutoka kwake na ninakushauri urudi Tanzania, kwani ulikokwenda ulikuwa umepotea njia,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, alimtaka Lembeli kurudi CCM kwani huko alikoamua kwenda, ndiko kwa sasa walipo hao mafisadi ambao alikuwa akiwazungumzia kila siku.

“Ninakuomba Lembeli urudi kundini, mimi ninakujua unavyowapenda wananchi wako wa Kahama na ukirudi sitakukata mkia kwani huko ulikokwenda umepotea njia na mimi ndio mwenyekiti ninayekuwa ninapigania wanachama wasaliti ambao asubuhi wapo CCM jioni wapo Upinzani,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Lembeli alisema aliamua kujitoa CCM na kujiunga na Chadema kwa madai chama hicho kumekithiri kwa rushwa, ufisadi pamoja na unafiki.

“Iwapo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa ambaye ni Rais John Pombe Magufuli atakisafisha chama hicho, basi na mimi ninaweza kurudi katika chama hicho kwa lengo la kuwahudumia wananchi,” alisema Lembeli aliyeshindwa uchaguzi mwaka jana na mgombea wa CCM, Jumanne Kishimba.

Alisema anashukuru Rais Magufuli kwa kuja Kahama na kuongeza kuwa yeye hana kinyongo na wataendelea kusalimiana, kwani kubadilisha msikiti sio mwisho wa Uislamu.

Aidha, alisema kama Rais Magufuli akikisafisha chama hicho, hana budi kurudi kundini kwani kwa sasa bado anasubiri kiongozi huyo kukisafisha chama hicho, kwa kuwa kimejaa watu ambao hawana sifa ya kukiongoza.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema yote aliyoyaahidi atayafanyia kazi na kuongeza kuwa hatalewa madaraka ya Urais na kuwataka Watanzania kumtanguliza Mungu katika kazi wanazozifanya za kila siku.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi wilayani Kahama, Rajabu Yahaya alimpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani kazi anazozifanya, ndio walizokuwa wakizipigania wapinzani katika majukwaa na kumtaka kuendelea kutumbua majipu.

Akizungumzia masuala mengine, Rais Magufuli aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya nchini kuacha kuwatoza ushuru wafanyabiashara ndogo kwani wao wao ndio waliosababisha CCM kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema aliomba kiti hicho kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi; na kuongeza kuwa ushuru au kodi ilipwe kwa watu wanaomiliki maduka na wafanyabiashara wakubwa waliopo katika maeneo husika.

Aidha, alisema katika uongozi wake hajaagiza wananchi wa kawaida walipe kodi, bali alitaka wananchi waishi maisha ya amani hasa wafanyabiashara ndogo ambao ndio walio wengi katika jamii iliyopo nchini.

Akiwa Isaka, Rais Magufuli alisema hatalipa fidia kwa nyumba takribani 300 kwa sasa, badala yake kazi kubwa atakayoifanya ni kuhakikisha anamaliza tatizo la maji katika mji huo, ambalo linawasumbua wananchi kwa muda mrefu. Imeandikwa na Raymond Mihayo na Kareny Masasi.

No comments