Header Ads

Waziri Mkuu Afafanua Kuhusu Kutenguliwa Kwa Uteuzi Wa Waziri Kitwanga

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Rais Dk. John Pombe Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Charles Kitwanga umefuata kanuni za utumishi wa umma ambao unakataza mtumishi kulewa akiwa kazini.

“Zipo sheria za utumishi ambazo mtumishi hatakiwi kunywa pombe na wala hapaswi kulewa akiwa kazini… mtumishi anapaswa kuwa na akili timamu inayokuwezesha kufanya kazi za Serikali,” alisema.

Ametoa ufafanuzi leo usiku (Ijumaa, Mei 20, 2016) wakati akijibu swali la mwandishi wa TBC1 aliyetaka kujua kama taarifa zilizoenea kuhusu kutenguliwa kwa Waziri huyo ni za kweli.

“Ni kweli Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Charles Kitwanga kuanzia leo tarehe 20 Mei, 2016 baada ya kuonekana amelewa wakati wa kazi. Na hili lilibainika pale alipokuwa akijibu maswali ya wizara yake leo asubuhi,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema kuna swali aliloulizwa ambalo hakulijibu vizuri na kwamba swali hilo litapaswa kurudiwa kuulizwa baada ya wabunge kuomba muongozo wa swali hilo.

IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU,
S L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, MEI 20, 2016

No comments