Header Ads

Serikali Yawatoa Wasiwasi Wananchi Kuhusu Uhaba wa Mafuta ya Ndege

SERIKALI imewatoa wasiwasi Watanzania kuhusu taarifa za kutokea kwa uhaba wa mafuta ya ndege, uliokuwa ukitishia kusimama kwa usafiri huo muhimu kwa nchi.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema hayo bungeni jana jioni wakati alipokuwa akihitimisha mjadala wa Bajeti ya wizara hiyo, alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo).

Awali Zitto katika hoja yake, alisema kuwa akiba ya mafuta ya ndege nchini imebaki ya siku tano, jambo linaloweza kusababisha ndege za kimataifa kushindwa kutua nchini.

“Zimebaki siku tano mafuta ya ndege aina ya JET AI kumalizika nchini baada ya mafuta yote kugundulika kuwa yamechafuka. Sasa baada ya siku hizo, ndege hazitatua nchini na itakuwa ni aibu na nchi itakosa fedha za kigeni kwa watalii kutokuja nchini,” alisema Zitto.

Alisema anazo barua kutoka kwa Wakala wa Kuagiza Mafuta kwa Pamoja na alikuwa tayari kuziwakilisha kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. 

Uchunguzi
Hata hivyo uchunguzi wetu, umebainisha kuwa kuna mafuta ya siku 15.

Taarifa kutoka vyanzo vinavyohusika na upokeaji wa mafuta nchini, hadi kufikia jana akiba ya mafuta ya ndege JET AI yanayofaa kwa matumizi ilikuwa lita 8,749,810 wakati yale ambayo ubora wake haufai, yalikuwa lita 28,131,341.

Taarifa hiyo ilionesha kuwa Puma Energy Tanzania ina lita 4,596,391, Oilcom (T) Ltd lita 256,842, Total (T) Ltd lita 2,715,516 na Gapco (T) Ltd lita 1,181,061. Kati ya lita 28,131,341 zenye ubora usiofaa, lita 14,432,736 zipo Puma Energy Tanzania, lita 10,840,059 ziko Oilcom (T) Ltd na lita 2,858,546 ziko Gapco (T) Ltd.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, matumizi ya mafuta ya ndege kwa siku ni lita 571,484, hivyo mafuta yaliyopo kutosheleza kwa siku 15 kuanzia jana. 

Aidha, ilifahamika kwamba mafuta ya ndege hayo aina ya JET AI yanayofaa kwa matumizi yanayosafirishwa kwenda kwa SP Rwanda ambayo yako katika ghala la Gapco ni lita 3,474,781.

Taarifa ya Waziri 
Akitoa majibu ya Serikali, Profesa Muhongo alisema mafuta yaliyopo yanatosha kwa siku 16 na tahadhari zote zimechukuliwa, kuhakikisha yataendelea kuwepo mpaka hapo shehena nyingine ya mafuta hayo itakapoingia katikati ya Juni mwaka huu.

Alisema wakati tahadhari hizo zikiwa zimechukuliwa, Shirika la Viwango (TBS), limeanza kufanya uchunguzi wa kilichotokea katika shehena ya mafuta yaliyochafuka, kwa kuwa yaliagizwa kwa pamoja lakini ajabu baadhi yalikutwa machafu na mengine masafi, huku akimwambia Zitto kuwa aliyempa taarifa, ni mmoja wa wenye mafuta machafu.

Mchango wa Zitto 
Katika mchango wake mwingine, Zitto alitaka kuongezwa kwa nguvu katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini, akisema kuna tatizo la kampuni kubwa kutumia njia za kihasibu kuhamasisha kwenda kule zilikosajiliwa.

Alitaka pia kuwapo kwa uangalifu katika kushughulikia mikataba ya uzalishaji umeme ili kuepuka taifa kuja kulipa fedha nyingi kama ilivyokuwa kwa Kampuni ya Dowans. 

Pia alipendekeza kuwapo kwa mapitio ya sheria ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ili isaidie kukusanya mapato zaidi katika madini.

Alishauri suala la mafuta na gesi kutokuwa la Muungano, kurekebishwa katika sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu bado halijafanyika hivyo, licha ya Zanzibar sasa kuwa tayari kushughulikia masuala hayo kama nchi.

No comments