Header Ads

Ofisa elimu ajinyonga Muleba



Muleba.  Katibu wa Tume ya Utumishi na Nidhamu ya Walimu (TSD ) Wilaya ya Muleba, Manase Mkumbo amekutwa amefariki dunia kwa kujinyonga shambani mwake katika Kijiji cha Kyamyorwa wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Francis Isack amesema Mkumbo alijinyonga usiku kuamkia leo.

Amesema kabla ya tukio hilo alituma ujumbe  wa maandishi kwa simu akimjulisha  mwanae aliye masomoni kuwa amekata tamaa na maisha.

Isack amesema Mkumbo aliondoka Muleba kwenda kukagua mashamba yake kijijini ambako aliandika  ujumbe huo na kununua kamba ya katani na kujinyonga.

Ujumbe huo ulipomfikia mtoto wake aliutuma tena nyumbani katika Kitongoji cha Bugombe wilayani Muleba ndipo wakaanza kufuatilia kwa kuwa alikuwa amewaaga kuwa anaelekea shambani ambako walikuta mwili wake umetundikwa.

“Inasikitisha mtu alibakiza mwaka mmoja astaafu  na kupata mafao yake lakini anaamua kujiondoa na kuacha hasara na simanzi kwa familia,” amesema Isack.

Amesema taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kwao mkoani Singida zinaendelea.

No comments