Header Ads

Mbunge Apinga Wakunga Wanaume Kuruhusiwa Kuwahudumia Wanawake Wakati wa Kujifungua


Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Riziki Mngwali amepinga mpango wa Serikali kuajiri wakunga wanaume katika baadhi ya zahanati kuhudumia wajawazito wakati wa kujifungua kuwa ni udhalilishaji dhidi ya wanawake.

Mbunge huyo ameitaka Serikali kuzingatia mila za Kiafrika, akisema imezoeleka kuwa huduma ya ukunga kwa wajawazito wakati wa kujifungua hutolewa na wataalamu wanawake.

“Serikali haioni kuwa kwa kuweka wakunga wanaume katika baadhi ya zahanati zake nchini ni kuwadhalilisha wajawazito wanaojifungua?”alihoji Mngwali.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jaffo alisema wakunga wanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga inayowataka kutoa huduma ya kumsimamia mjamzito wakati wa uchungu, kujifungua na baada ya kujifungua bila kujali jinsia.

Alisema pamoja na sheria hiyo, kumekuwa na changamoto zinazotokana na mila na desturi za jamii ambazo husababisha baadhi ya wahitaji wa huduma hiyo kutokubali kuhudumiwa na wakunga wanaume.

“Kutokana na hali hii, Serikali itaendelea kuajiri wataalamu wengi ili pale penye changamoto paweze kupatiwa ufumbuzi bila kukwaza jamii husika,” alisema Jaffo.

Naibu waziri alisema hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa mbunge huyo kuuliza swali hilo bungeni, lakini tayari amewasiliana na uongozi wa Mkoa wa Pwani ambao umeeleza kuanza kulifanyia kazi jambo hilo na kwa baadhi ya maeneo wameshaanza kupeleka wakunga wanawake.

No comments