Header Ads

LHRC Yaonya Kuhusu Picha za Uchi na za Kutisha

Kituo  cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeonya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu kuchapisha picha za utupu ama za kutisha katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam , Mkurungenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Dk. Helen Kijo Bisimba alisema kuwa, kumekuwa na matukio kadha yanayofanywa na watu juu ya kurekodi na kupiga picha ambazo sio nzuri kwa mujibu wa sheria.

Alibainisha picha hizo kuwa ni pamoja na matukio ya mauaji, ajali za kutisha na miili ya marehemu zinazochapichwa katika mutandao ya kijamii, blog na hata baadhi ya vyombo vya habari bila kijali kwamba, kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Dk. Kijo alisema kuwa, tarehe 4 Mei mwaka huu katika Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Bagamoyo picha za miili ya marehemu (mama na mtoto) ambayo majina yao yamehifaziwa, zilisambazwa katika mitandao ya kijamii zikionesha majeraha ya kutisha   kutokana na kitendo cha kinyama kilichofanywa.

Katika tukio la pili alibainisha kuwa, ilitokea Mkoa wa Kilimanjaro mwaka huu ambapo picha za maiti ya mtoto aliyeuawa na mama wa kambo zilionesha akiwa ndani ya jeneza.

Katika maeneo ya Kibamba Jijini Dar es Salaam, Januari mwaka huu picha za utupu za mwanamke aliyesemekana kuwa ni msukule aliyekutwa kwenya kisima zilizambazwa katika mitandao ya kijamii.

Alisema kuwa, hayo ni baadhi ya matukio hivyo jamii inapaswa kutambua kuwa vitendo hivyo ni udhalilishaji na kinyume cha sheria.

“Kwani kwa mujibu wa haki ya kikatiba ibara ya 16 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 kila mtu ana haki ya kikatiba ya kuthamini utu wake kuwa faragha akiwa hai au amefariki,” alisema.

No comments