Kasi ya Watanzania Kujiunga na Makundi ya Kigaidi ya Al-Shabaab na IS Yaongezeka........Waziri Asimulia Wanavyojiunga, Wapinzani Wahoji Wanajeshi Kupewa Ukuu wa Mikoa
Serikali imesema imeshtushwa na wimbi kubwa la vijana wa Kitanzania wanaojiunga na makundi hatari ya kigaidi ya Al-Shabaab na Islamic State, maarufu kama ISIS.
Kauli hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake ya Sh trilioni 1.6 kwa mwaka 2016/17.
Dk. Mwinyi alisema pamoja na hali hiyo, Serikali imeendelea kupambana na makundi hayo kwa kila njia ili kuhakikisha nchi inakuwa salama katika maeneo yote, yakiwamo ya mipakani.
Alisema matukio ya kigaidi yameendelea kuwa tishio duniani, hivyo Tanzania inapaswa kuchukua tahadhari ya kila namna.
Dk. Mwinyi alisema kuwapo kwa makundi hayo ya Al-Shabaab, Al-Qaeda, Boko Haram na Islamic State, kunafanya tishio la ugaidi kusambaa duniani kote.
“Taarifa za kuwapo baadhi ya Watanzania wanaojiunga na makundi ya Al-Shabaab na ISIS tunazo, kunahatarisha usalama wa Tanzania, hasa ikizingatiwa kiujumla mwingiliano mkubwa uliopo kati ya wananchi wetu na watu wenye malengo tofauti.
“Hatari iliyopo ni uwezekano wa baadhi ya vijana waliojiunga na makundi ya kigaidi ya kimataifa kurejea nyumbani kwa lengo la kutekeleza vitendo vya kigaidi nchini mwetu.
“Tuna kila sababu ya kujizatiti na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama,” alisema Dk. Mwinyi.
Alisema kipindi kilichopita, kumejitokeza viashiria vyenye mwelekeo wa kigaidi, ikiwemo kuvamiwa baadhi ya vituo vya polisi, kuporwa silaha na baadhi ya askari kuuawa na kundi ambalo nia yake haijafahamika.
“Matukio yenye mwelekeo wa kigaidi, ni kama yaliyotokea katika mapango ya Amboni mkoani Tanga, Kitongoji cha Nyandeo wilayani Kilombero pale Morogoro na kukamatwa mabomu ya kutengenezwa kwa mkono katika maeneo mbalimbali yakiwamo Zanzibar,” alisema.
Alisema pamoja na hali hiyo, kwa upande wa mpaka wa kusini mwa nchi, hali imeendelea kuwa shwari, licha ya uwapo wa utata wa mpaka wa Ziwa Nyasa ambao bado haujapatiwa suluhisho.
Kutokana na hali hiyo, amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kwa kutoa taarifa ya matukio yanayotishia kuashiria uvunjifu wa usalama.
Kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana na ule wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu Zanzibar, alisema umefanyika kwa amani na utulivu, licha ya baadhi ya maadui wa ndani na nje kutabiri mambo mabaya.
“Watanzania tunayo sababu ya kujivunia kuwa uchaguzi mkuu ambao kikalenda ni wa tano tangu kuingia mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, uliendeshwa na kuhitimishwa kwa amani, utulivu na mshikamano mkubwa kinyume na maadui wetu wa ndani na nje ya nchi waliotutabiria mabaya,” alisema.
Dk. Mwinyi alisema kwa kutambua umuhimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana, Serikali itaendelea na azma yake ya kuwajenga vijana uzalendo, ukakamavu, maadili mema, utaifa na kutoa stadi za kazi.
Alisema kutokana na uwezo mdogo wa kifedha, suala hilo sasa litatekelezwa kwa kutoa mafunzo kwa baadhi ya vijana wa kujitolea kwa mujibu wa sheria.
“Katika mwaka 2015/16, vijana 27,463 walipatiwa mafunzo mbalimbali, yakiwamo ya kuwapa ujuzi na stadi kazi ili wajiandalie mazingira mazuri ya kujiajiri.
“Nachukua fursa hii kuwaomba vijana wanaopata mafunzo ya JKT, wazingatie maarifa na ujuzi wanaoupata, hususan wa stadi za kazi ili waweze kujiajiri badala ya imani iliyoanza kujitokeza kwa baadhi ya wahitimu kudai ajira kwa maandamano.
“Katika hatua ya kutekeleza agizo la Serikali linalohusu vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuajiri idadi kubwa ya vijana wanaopatiwa mafunzo ya JKT, hadi kufikia Februari, mwaka huu vijana 5,453 waliajiriwa na vyombo vya ulinzi.
“Kati ya vijana hao, 3,521 waliajiriwa na JWTZ, polisi 1,185, Usalama wa Taifa 106, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) 617. Hata hivyo, idadi ya vijana waliopatiwa ajira imeongezeka. Hadi kufikia Aprili, mwaka huu vijana 7,170 wamejiariwa na vyombo hivyo,”alisema Dk. Mwinyi.
==>Kambi ya upinzani wahoji wanajeshi kupewa ukuu wa mikoa
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, msemaji wa wizara hiyo, Juma Hamad Omar, alihoji hatua ya Serikali kuwateua maofisa wa vyombo vya ulinzi kushika nafasi za kisiasa kama wakuu wa mikoa na wilaya.
Omar ambaye ni Mbunge wa Ole (CUF), alisema Serikali imekuwa na utamaduni wa kuwateua maofisa wa vyombo vya dola waliopo kazini, na baada ya uteuzi huo hufanya kazi kwa mujibu wa chama tawala.
“Wakuu wa wilaya na mikoa wanafungwa na ibara ya 80 (1) (C) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 inayowataja kuwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM katika wilaya husika. Hali kadhalika wakuu wa mikoa wanafungwa na ibara ya 94 (1) (C) inayowataja kuwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM katika mkoa husika.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali itambue ibara 147 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka kwamba; ‘Itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kama atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara 5 ya Katiba hii’,” alisema Omar.
Akizungumzia utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo, alisema katika bajeti ya mwaka 2015/16 Serikali imeweka rekodi mbaya ya kutoa fedha chini ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge kwa miradi ya maendeleo.
Post a Comment