Chadema wabeza utumbuaji majipu wa Magufuli, wadai bora Kikwete
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Vincent Mashinji ameponda mtindo wa utawala wa Rais John Magufuli wa utumbuaji wa majipu akisema umekosa dira na kinachoendelea ni utashi wa kisiasa na kukurupuka.
Kazi kubwa aliyoifanya Rais Magufuli tangu aingie madarakani, katika kipindi cha miezi sita sasa ni kubana matumizi ya fedha za umma kwa kufuta safari za nje za watumishi, kuzuia mikutano kufanyika mahotelini, kuhimiza mamlaka husika kukusanya kodi, kupambana na watumishi hewa, kuwasimamisha au kutengua uteuzi wa watendaji aliodai kuwa ni wazembe na walioshindwa kwenda na kasi yake pamoja na kuwashughulikia wala rushwa na wahujumu uchumi.
Katika namna inayoonekana ni kufuata upepo wa kisiasa, Rais Magufuli huwatumbua baadhi ya watendaji kwenye mikutano ya hadhara.
“Kuna vitu vingi vinafanyika lakini hatujui kipi ni kipi na wapi tunaelekea. Kuna mambo mengi yanafanyika, lakini hakuna hata mtu mmoja katika nchi hii anayejua Taifa hili lina mpango gani na linaelekea wapi,” Mashiji anakaririwa na gazeti la Mwananchi.
Huku akifananisha utawala wa Rais Magufuli na wa mtangulizi wake Jakaya Kikwete, Dk Mashinji alisema walau ahadi ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania” ilikuwa inaeleweka hata kama haikutekelezeka.
“Rais Kikwete alitwambia Maisha bora kwa kila Mtanzania na tulijua maisha hayo yanapatikana kwa kupambana wenyewe na tulipambana. Lakini sasa hatujui tunaelekea wapi. Hapa kazi tu! Umemfukuza huyu kazi halafu nini kitaendelea? Keshaondoka kakuacha, unaajiri mwingine? Tunahitaji mtu wa kujibu hayo maswali. Nchi yote sasa inavurugwa. Halmashauri zinavurugwa,” alisema.
Katibu mkuu huyo alisema kwa sasa kila kitu kinavurugwa jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa nchi na kwamba inaonekana wazi nchi inaelekea sehemu ambayo mbele kuna giza.
Akitoa mfano wa mfumo ulivyobadilika alisema hivi sasa wakurugenzi wa halmashauri wametangaziwa kusitisha mawakala wote wanaokusanya ushuru badala yake wakusanye wenyewe.
“Hivi tujiulize halmashauri ina wafanyakazi wangapi ambao wana uwezo wa kukusanya mapato yake? Huku ni kudanganyana,” alisisitiza Dk Mashinji.
Hata hivyo, Dk Mashinji alisema hawapingi anachokifanya bali tofauti yao na Rais Magufuli ni namna ya kukabiliana na jambo.
“Sisi tunaamini katika mfumo na siyo mtu. Huwezi leo kuniambia meya anaiba Sh5 bilioni halafu chama kisijue. Kwa nini chama kisimwondolee udhamini kabla?” alihoji.
“Anachofanya sasa ni kudhibiti na siyo kurekebisha mfumo. Rais Magufuli hana dhamana na Mungu, asipokuwepo sioni wa kuendeleza falsafa zake. Kwa nini kusiwe na mfumo madhubuti ambao upo kisheria na kila mmoja aujue na kuufuata?” alieleza.
Post a Comment