Header Ads

Afungwa miaka 30 kwa utekaji magari


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemhukumu Joseph Ugali (30) kifungo cha miaka 30 jela na viboko 12 baada ya kupatikana na kosa la utekaji wa magari.

Akitoa hukumu hiyo juzi, Hakimu wa Wilaya, Leonard Nkola, alisema Mahakama imemtia hatiani Ugali hivyo atakwenda jela miaka 30 na kuchapwa viboko 12 iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.

Hakimu Nkola alisema kwamba vitendo vya uhalifu, vimeshamiri katika wilaya ya Igunga na adhabu hiyo kali itafanya watu wengine wenye nia ya vitendo hivyo kuacha.

Awali, Mwendesha Mashitaka wa Polisi wa wilaya hiyo, Edwini Sempoly alidai mahakamani kuwa mtu huyo alitenda kosa hilo Novemba 3 mwaka 2015 saa 6:30 usiku katika kijiji cha Igogo maeneo ya darajani, kata ya Nanga wilayani hapa.

Alidai siku hiyo ya tukio, Ugali, mkazi wa kijiji cha Bulyang’ombe akiwa na wenzake watatu, Maiko Ezekiel, Mohamed Athuman na Abdul Ramadhani, walifunga barabara kuu ya Mwanza-Dar es Salaam kwa kuweka vizuizi vya magogo na mawe barabarani.

Kwamba baada ya kufunga barabara hiyo, mtu huyo na wenzake walizuia magari aina mbalimbali na kuwapora baadhi ya abiria wa magari hayo Sh milioni 2.15 na simu sita za aina mbalimbali.

Baada ya washtakiwa kusomewa mashitaka, walikana kutenda kosa hilo. Upande wa mashitaka ulipeleka mashahidi na kumtambua mshtakiwa Joseph Ugali kati ya hao wanne. Mahakama iliwaachia washtakiwa watatu baada ya kuwaona hawana hatia kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha juu ya tuhuma zinazowakabili.

No comments