DARAJA LA KIGAMBONI KUANZA KUTUMIKA.
WAKAZI wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake kesho watapata fursa ya kulitumia kwa mara ya kwanza daraja la Kigamboni. Daraja hilo linatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais John Magufuli, Jumanne, wiki ijayo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mradi kutoka kampuni ya China Railway Construction Engineering Group ambao wametekeleza mradi huo kwa ushirikiano na kampuni ya China Railway Major Bridge Group, Zhang Bangxu, alisema kesho wataruhusu wakazi hao na magari kupita bila kutozwa fedha katika daraja hilo lililojengwa kwa Dola za Kimarekani milioni 135.
“Tutaruhusu magari kupita kwenda upande wa Kurasini na upande wa Kigamboni kesho kutwa (kesho) tu kama maandalizi ya sherehe za ufunguzi na pia kutuwezesha kufanya majaribio ya mitambo na mashine zote ambazo zitatumika katika kufanya tozo mbalimbali,” alifafanua.
Kwa mujibu wa Zhang, daraja la Kigamboni ndiyo daraja refu kuliko yote katika ukanda wa Afrika Mashariki lililotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya matumizi ya kamba kubeba uzito wa daraja, ambalo litaunganisha jiji la Dar es Salaam na eneo la Kigamboni na Kurasini.
Ujenzi ulianza Februari Mosi mwaka 2012. “Pamoja na kujengwa katika ubora wa hali ya juu, daraja hili lina jumla ya njia sita, yaani njia tatu kwa kila upande, pamoja na njia mahususi kwa ajili ya waenda kwa miguu na waendesha baiskeli ambayo ina upana wa mita 2.5 katika kila upande.
Daraja hilo litaruhusu magari yenye uzito usiozidi tani 30 kupita,’’ alisisitiza Zhang. Alisema kaskazini mwa daraja hilo, litaungana na barabara yenye urefu wa kilometa moja inayokatiza katika reli ya Tazara kisha kuungana na barabara ya Mandela. Kwa upande wa Kigamboni, daraja litaungana na barabara yenye urefu wa kilometa 1.5 ambayo inaungana na barabara ya Kigamboni Ferry - Kibada.
Post a Comment