Header Ads

Ashikiliwa na Polisi kwa Kumtukana Rais Magufuli


Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, limemkamata Isaack Habakuk Emily, kwa kosa la kumtukana Rais John Magufuli kuwa ni bwege na kwamba hawezi fananishwa na Nyerere na kusambaza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza ofisini kwake, leo jijini Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 22 mwaka huu eneo la Hotel ya Anex jijini humo.

Amesema kuwa baada ya kumkamata alifanyiwa upekuzi na kukutwa na simu ya kiganjani aina ya Tecno iliyotumika kutenda kosa la kutuma ujumbe wa kumkashifu Dkt. Magufuli.

Mkumbo amesema kuwa mtuhumiwa huyo alituma ujumbe wa kashfa kwenye Facebook usemao:- “Mnamlinganishaje Magufuli na Nyerere,” na kutuma kwa watu mbalimbali kupitia simu yake ya mkononi.

Mkumbo amesema mtuhumiwa baada ya kusikia hivyo aliandika tena ujumbe kwenye mtandao wake usemao, “Hizi ni siasa za maigizo halafu mnamfananisha huyu bwege na Nyerere wapi Bwana,” amesema.

Amesema baada ya kutuma ujumbe huo uliwaudhi watu wengi waliopokea ujumbe huo na kuwakwaza, hali iliyosababisha kupeleka malalamiko yao Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mamlaka hiyo ilitoa taarifa polisi na hatua za kisheria zilianza kuchukuliwa.

Aidha amesema baada ya hapo walifanikiwa kumpata mtuhumiwa wa uhalifu kwa njia ya mtandao, kumtia hatiani na jana alifikishwa mahakamani kujibu shitaka lake.

Hata hivyo Jeshi la Polisi limetoa rai wa watu wote kutumia mitandao ya kijamii vizuri kwa kujiletea maendeleo na kubadilishana taarifa zenye tija na siyo zenye kuvunja sheria.

Pia amesema Jeshi hilo limejipanga kuwatia nguvuni wale wote watakaovunja sheria kwa kutumia mitandao ya kijamii.

No comments