Header Ads

Tanzania imepoteza asilimia 60 ya tembo kwa ujangili

Tanzania imepoteza asilimia 60 ya tembo tangu mwaka 2009, huku mamia ya tani za pembe za ndovu yakipelekwa kinyemela China na maeneo mengine duniani.

Hayo yalisemwa jana na Meneja Mradi wa Shirika la Kimataifa la Wanyamapori (WildAid), Salome Gasabile wakati wa uzinduzi wa video ya wimbo wa kutokomeza biashara ya pembe za ndovu na ujangili.

Gasabile alisema mwaka 2009 kulikuwa na takribani tembo 110,000, lakini hadi kufikia mwaka 2014 idadi wanyama hao ilipungua na kubaki 43,000.

Video hiyo inayoitwa Lupela imetolewa na msanii Ali Kiba, mahususi kwa ajili ya kupiga vita mauaji ya tembo yanayofanywa na majangili.

“Tunajivunia kuwa na msanii Ali Kiba kama balozi wa WildAid, kwani mwaka uliopita, alikuwa akifanya kazi kwa bidii bila kuchoka kwa ajili ya tembo na tunaamini kwamba wimbo huu utaleta hamasa kubwa,” alisema.

Alisema video ya wimbo huo ilitengenezwa na kurekodiwa na Brian Rumsey na kusimamiwa na Oththan Burnside aliyefanya kazi na wasanii maarufu duniani Rihanna na Sean Paul.

Gasabile alisema chini ya kauli mbiu ya ‘Ujangili unatuumiza sote’ Ali Kiba amekuwa akifanya kazi sambamba na WildAid kuhamasisha wananchi kupambana na ujangili wa tembo ambao umesababisha maelfu kuuawa kikatili kwa ajili ya pembe zao.

Ali Kiba aliahidi kuendelea kuwalinda tembo waliopo nchini ili kutokomeza biashara ya pembe za ndovu kama nchi nyingine zinavyofanya.

“Nina furaha kutoa wimbo mpya, lakini najivunia kwamba Lupela imewalenga zaidi tembo wa Tanzania, natumaini mashabiki wangu wote watauona uhitaji mkubwa wa kuwalinda tembo wetu na kutokomeza biashara ya pembe za ndovu,” alisema.

No comments