Mama Amuua Mwanae Kwa Kichapo Na Kisha Kuitundika Maiti Yake Mtini.
Mtoto wa miaka 11, Nchambi Tungu, ameuawa kikatili na mama yake mzazi kwa kuchapwa fimbo kisha kumfunga kamba shingoni na kumning’iniza kwenye tawi la mwembe ili ionekane kuwa amejinyonga mwenyewe.
Inaelezwa kuwa mama wa mtoto huyo, Sado Roketi (26) mkazi wa kitongoji cha Mnyakasi, kijijini Ikuba, wilayani Mlele, mkoa wa Katavi alimuua mwanawe huyo baada ya kukataa kumfulia nguo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, jana alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.
Alisema tukio hilo ni la Januari 23, mwaka huu saa moja jioni katika Kitongoji cha Mnyakasi. Alisema siku ya tukio mtuhumiwa alimpatia mwanawe huyo nguo amfulie lakini mtoto huyo alikataa kuzifua akaendelea kucheza na wenzake.
“Ndipo mama huyo kwa hasira alipoamua kuchukua fimbo na kuanza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia kifo, aliubeba mwili na kuutundika kwenye matawi ya mti wa mwembe baada ya kumfunga kamba shingoni na kumwacha akining`inia ili ionekane alijinyonga mwenyewe,” alieleza Kidavashari .
Alisema mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Post a Comment