Header Ads

TUMIENI TEKNOLOJIA MIKUTANO KWA NJIA YA VIDEO ILI KUOKOA GHARAMA – MKURUGENZI MTENDAJI WA TAGLA.

UT3Mkurugenzi Mtendaji  Wakala wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao Bw.Charles Senkondo  akizungumza na waandishi wa habari (ambao hawapo katika  picha) baada ya kumalizika kwa Mkutano  na Sekretarieti za Mkoa kwa njia ya Video  jana jijini Dar es Salaam.
UT1Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma Bw.Peter Mushi (wa pili kushoto) akizungumza alipokuwa akiendesha  mkutano kwa njia ya video na Sekretarieti ya Mkoa wa Mara jana jijini Dar es Salaam (watatu kulia) ni Mkurugenzi Msaidizi  Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma Bw. Leonard Mchau .
UT2 Baadhi ya watendaji kutoka wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma  wakiendelea na  Mkutano kwa njia ya Video  na Sektertarieti za Mikoa ya Lindi,Mara,Geita,Singida na Shinyanga jana jijini Dar  es Salaam.
……………………………………………………………………………………………
Na Anna Nkinda – Maelezo
  Watanzania wametakiwa kutumia technolojia ya mawasiliano ikiwemo kufanya mikutano kwa njia ya video ambayo itawaondolea gharama ya kusafiri na hivyo kuokoa fedha  na muda.
Rai hiyo imetolea   hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Charles Senkondo wakati akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kazi wa video conference kati ya Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Taasisi zake, Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za mitaa.
Senkondo alisema kufanya mikutano kwa njia ya video kunamfanya mtu asisafiri na hivyo kuepukana na ajali, kutopoteza muda awapo safarini na na kupata wasaa wa  kukaa na familia yake.
“Kuanzishwa kwa TaGLA kumeongeza uwezo wa kufanya kazi kwa ubunifu zaidi, kwa njia ya kisasa, kwa maamuzi zaidi ya kiuendeshaji kwa kuangalia kila mara mahitaji ya wadau na kutumia mbinu za soko katika utoaji wa huduma bora”.
“Kabla ya kukuwa kwa teknolojia watu walikuwa wanasafiri umbali mrefu kwenda kushiriki mikutano hivi sasa wamepunguza safari zisizo na umuhimu.  Mtu atasafiri katika mikutano ya umuhimu tu zamani ilikuwa lazima mtu aje sasa hivi anafuatwa popote alipo na kuletwa katika video conference”, alisema Senkoro.
Akiongelea kuhusu kituo hicho Mkurugenzi huyo alisema zaidi ya washiriki elfu 20 wameshiriki midaharo na mafunzo 783 ya  kubadilishana maarifa kupitia Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao (TaGLA) .
Senkondo alisema wakala hiyo imeweza kutoa mafunzo kwa viongozi wakiwemo mawaziri, wakuu wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi na kuleta urahisi wa vikundi na watu waliotengwa kijiografia kuonana, kusikilizana na kukubaliana kwa wakati mmoja.
“Wakala kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kutumia mitandao ya teknolojia imeweza kufundisha watendaji wakuu wa Taasisi za Serikali, wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya zote na wakurugenzi wa rasilimali watu wapatao 1,200 mfumo wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali (HCMIS) Lawson version 7”, alisema Senkoro.
Mkurugenzi  huyo mtendaji alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni fikra potofu juu ya matumizi ya TEHAMA na kukubalika kwa kasi kwa teknolojia  na kuwaomba waandishi wa habari pamoja na wadau wengine kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya Tehama.
Senkoro alisisitiza, “Tunawaalika wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, waandishi wa habari, watu binafsi na asasi za jamii watumie huduma zetu ambazo tunazitoa kwa gharama naafuu kuweza kuwafikia wadau wengi kwa muda mfupi bila kujali umbali au changamoto za kijiografia.
Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao umewezesha kufanyika kwa mahakama kwa kutumia mikutano ya video katika kesi mbalimbali kwa kutoa ushahidi wake kwa njia ya video na kusaidia kupunguza gharama  na kuhamasisha maamuzi na hivyo utoaji wa haki katika kesi husika.
Mkutano huo wa kazi wa video conference kati ya Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Taasisi zake, Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za mitaa ulijumuisha viongozi wa Serikali kutoka mikoa ya Dodoma, Lindi, Geita, Singida, Pwani, Mara, Iringa, Mtwara, Shinyanga na Njombe.

No comments