JAMII YAASWA KUELEWA NA KUTETEA HAKI ZAKE.
Nami nikiwa mmoja kati ya waliofaidika na mafunzo hayo,kushoto ni Bi.Chitra Massey
Na Paul WilliamJamii imetakiwa kutambua haki zake kisheria.Hayo yamesemwa na Bi.Chitra Massey,mshauri mkuu wa haki za binadamu kutoka umoja wa mataifa(UN) wakati akiongea na waandishi wa habari na watangazaji wa kituo cha redio cha 88.9 STORM FM kilichopo mkoani Geita.
Bi.Massey ameanza kufundisha kwa vitendo ambapo aliwataka washiriki kusimama upande mmoja na baadae kuwapa vikaratasi ambavyo vilikuwa na maelezo tofauti ikiwa ni mfano halisi wa hali ya maisha katika jamii,kwenye karatasi hizo kuliandikwa maneno tofauti kama vile mbunge,Rais,mtoto wa tajiri,masikini mlemavu n.k.
Kila mmoja alitengwa kulingana na karatasi yake ilivyokuwa imeandikwa,na kupata makundi mawili yaliyowakilisha hali halisi iliyopo katika jamii(wenye navyo na wasio navyo)
Bi.Massey alisema kuwa hiyo ndiyo hali halisi ilivyo katika jamii,kuwa wapo wanaodhani kuwa wao ni bora zaidi kuliko wengine na hivyo hali hii imepelekea matabaka katika jamii duniani kote.
Akizungumzia haki za binadamu amesema kuwa binadamu wote ni sawa na hakuna aliye juu ya sheria,na kuongeza kuwa kila mtu ana haki ya kuishi,kupata elimu,chakula bora,maji safi,huduma nzuri za afya n.k
Aidha Bi.Massey amewaasa wanahabari kuwa msitari wa mbele katika kulinda na kutetea haki za watu,akitolea mfano kina mama waishio vijijini ambao kwa asilimia kubwa hawaelewi haki zao hujikuta katika masaibu makubwa kama kupigwa,kunyanyaswa kijinsia na kudhalilishwa lakini wamekuwa hawajui wapi pa kusemea matatizo yao.
Zipo haki nyingi za binadamu ambazo Tanzania imekwisha tia saini,lakini si zote!miongoni mwa haki hizo zipo zile za mapenzi na ndoa za jinsia moja na nyingine ambazo zilikataliwa, hata hivyo ameisifu serikali ya Tanzania kwa kutekeleza vizuri baadhi ya mikataba iliyoweka na Umoja wa mataifa akitolea mfano jinsi wakimbizi kutoka Burundi wanavyohifadhiwa vizuri na kuhudumiwa katika kambi za Nyarugusu mkoani kigoma.Amewataka waandishi wa habari kuwa mabalozi na kuchukua jukumu la kuwasemea wanyonge ili kufikia malengo ya milenia ya umoja wa mataifa kuwa baada ya miaka kadhaa ijayo pasiwepo mtu yeyote atakaye achwa nyuma.
Naye mkurugenzi wa 88.9 STORM FM Bwana Santa Chacha amemshukuru Bi.Chitra Massey kwa kufika kwake na kutoa mafunzo hayo ambayo yameongeza uelewa na kujitambua kwa wanahabari wa kituo hicho,na kumtaka wakati mwingine kurudi pindi apatapo nafasi kuja kutoa elimu hiyo zaidi.
Kwa maelezo zaidi kuhusu haki za binadamu unaweza kutembelea WWW.OHCHR.ORG
Post a Comment