Header Ads

BURUNDI:NKURUNZINZA AAPISHWA KINYEMELA.


Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ameapishwa jana, siku sita kabla ya tarehe rasmi kulingana na katiba ya nchi hiyo ambapo alitarajiwa kuapishwa mnamo tarehe 26 mwezi Agosti.

Taarifa kutoka ofisi ya Rais imesema Nkurunziza ameapishwa rasmi jana kuwa rais wa nchi hiyo kwa muhula mpya wa miaka mitano ijayo. Sherehe hiyo ya kuapishwa kwa kiongozi huyo wa Burundi imekuja ghafla na kutangazwa saa chache kabla ya sherehe yenyewe kufanyika.

Maofisa wa kijeshi waliagizwa jana asubuhi kuvalia sare zao rasmi na kufika bungeni kwa ajili ya sherehe hizo za ghafla za kuapishwa kwa Rais Nkurunziza. Hakuna viongozi kutoka nchi za kigeni ambao wamealikwa kuhudhuria sherehe hizo za kuapishwa kwa kiongozi huyo wa Burundi.

Nkurunziza mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni kiongozi wa zamani wa waasi na aliyekuwa mwalimu wa michezo, aliingia kwanza madarakani miaka kumi iliyopita mwaka 2005 alipochaguliwa na bunge na kuchaguliwa na umma mwaka 2010.

Muhula wa tatu wa Nkurunziza umesababisha ghasia nyingi, kwa mujibu wa katiba ya Burundi, rais anastahili kukaa madarakani mihula miwili tu ya miaka mitano, lakini Nkurunziza na washirika wake wamedai muhula wake wa kwanza madarakani, alichaguliwa na bunge na sio umma na kwa hivyo anastahili kuendelea kuwa madarakani.

Uamuzi wake mwezi Aprili mwaka huu kuwa atagombea muhula wa tatu madarakani umezua mzozo mkubwa wa kisiasa na kusababisha ghasia nchini humo.

Nkurunziza alishinda muhula wa tatu baada ya uchaguzi wa rais uliofanywa tarehe 21 mwezi Julai ambao ulisusiwa na vyama vya upinzani nchini humo na mapema mwezi huu alitangazwa na tume ya uchaguzi nchini Burundi CENI kuwa mshindi kwa asilimi sitini na tisa ya kura zilizopigwa dhidi ya mpinzani wake wa karibu Agathon Rwasa ambaye licha ya kuususia uchaguzi huo alipata asilimi 18 ya kura zilizopigwa.

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Marekani zimesema chaguzi zilizofanywa nchini Burundi hazikuwa za huru na haki kwani mazingira hayakuwa salama na bora kuendesha chaguzi na kuhakikisha kila upande unashiriki kikamilifu.

Baraza la usalama la umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kisiasa na kiusalama katika taifa hilo dogo la Afrika Mashariki na kutoa wito pande zínazozana Burundi kufanya mazungumzo ili kuutatua mzozo huo na kuepusha taifa hilo kutumbukia katika vita.

Watu kadhaa mashuhuri nchini humo wametorokea nchiza kigeni wakihofia usalama wao na wengine waliosalia nchini humo wamelengwa kwa kuuawa, kushambuliwa, kukamatwa, kuteswa au kutishiwa maisha yao wakiwemo maafisa wa kijeshi,wanahabari na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu.

Milio ya raisasi imekuwa ikisikika karibu kila siku katika mitaa ya mji mkuu wa Burundi, Bujumbura huku askari na wanajeshi wakijaribu kuwakandamiza wanaompinga Rais Nkurunziza.

Mzozo huo wa Burundi unahofiwa kuwa huenda ukalitumbukiza taifa hilo tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kama vilivyoshuhudiwa kati ya mwaka 1993 hadi mwaka 2006 ambapo kiasi ya watu laki tatu waliuawa.

No comments