Header Ads

LOWASSA KUTOA TAMKO LEO KUHUSU HATIMAYAKE..


SASA ni rasmi kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa anajiunga katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na leo anatarajiwa kuzungumzia suala hilo, lililotanda katika siasa za Tanzania tangu baada ya kutopata nafasi ya kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wake wa urais.
Msemaji wake, Aboubakary Liongo alithibitisha jana jioni kuwa mbunge huyo wa Monduli, atazungumza saa 10 kamili jioni leo Dar es Salaam, kutoa kauli yake kuhusu mwaliko wa Ukawa, umoja ulioasisiwa wakati wa mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba mwaka jana, ukimwalika ajiunge nao.
Liongo alieleza kuhusu mkutano huo wa leo, baada ya wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa kuzungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi Kuu za Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni, Dar es Salaam na kuchukua fursa hiyo kumwalika Lowassa kujiunga nao na kumsafishia njia ya kuwa mgombea wao wa urais.
“Tunachukua fursa hii kipekee kumwalika Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mheshimiwa Edward Lowassa ajiunge na Ukawa na tuko tayari kushirikiana naye katika kuhakikisha tunaiondoa CCM madarakani katika Uchaguzi Mkuu ujao. “Tunaamini Mheshimiwa Lowassa ana uwezo wa kuhamasisha umma kuikataa CCM yenye kusimamia mifumo isiyotenda haki. Ni mchapakazi makini na mfuatiliaji wa karibu wa utendaji katika majukumu anayokabidhiwa,” alisema Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa wakati akisoma taarifa ya Ukawa.
Mbatia alisema ili kuleta mabadiliko yatakayowapatia Katiba bora na kufikia malengo, ambayo wameyaanisha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ni muhimu Ukawa ushinde uchaguzi wa 2015.
Alidai kuwa Watanzania wameshuhudia hadaa, uonevu, udhalilishaji, upendeleo na ukandamizaji katika mchakato wa kupata Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM.
“Kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu, kanuni na Katiba ya chama chao,” alidai Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa. “Katika kutafakari kwa kina maslahi mapana ya Taifa letu, Ukawa tunahitaji viongozi wenye sifa, uwezo na weledi katika kulinda, kuheshimu na kusimamia rasilimali za Taifa kwa maslahi ya Watanzania wote,” alisema Mbatia na kuongeza: “Viongozi wa aina hii hawawezi kuwa ndani ya CCM maana mfumo wa CCM haumpi kiongozi binafsi kutumia vipaji vyake au ubunifu wake binafsi katika kusimamia maslahi ya Taifa letu.”
Kwa mujibu wa Mbatia, Ukawa inayoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF, inaamini kuwa kwa maslahi mapana ya Taifa, wanamhitaji kila Mtanzania ambaye yuko tayari kujiunga nao katika kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa salama na lenye amani ya kweli ambayo msingi wake ni haki.
Kwa hiyo, alisema ni rai ya Ukawa kwa kila Mtanzania ambaye yuko tayari kushirikiana kuuondoa mfumo huo aliodai ni kandamizi na dhalimu wa CCM kushirikiana na Ukawa kwa lengo la kujenga Taifa imara.
Mbali ya Mbatia, wengine waliohudhuria mkutano huo ambao mwenyekiti huyo alisoma taarifa hiyo kwa dakika takriban 10 kuanzia saa tisa kamili alasiri, ni Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Makamu wake wa Zanzibar, Dk Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu wake Zanzibar, Said Issa Mohamed na Mwenyekiti wa Taifa wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Profesa Lipumba alidai kuwa masuala ya ufisadi ni masuala ya mfumo uliopo ambao ndio unaoleta ufisadi, na kwamba Lowassa mwenyewe alikwisha kuzungumzia suala la ufisadi akitaka mwenye ushahidi kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwake aweke hadharani.
Katika swali hilo, mwandishi alitaka kufahamu kuhusu hoja kuwa Lowassa ni fisadi na alihusishwa na kashfa ya Richmond iliyomfanya ajiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008.
“Suala la ufisadi ni suala linalosababishwa na mfumo uliopo, si suala la mtu mmoja mmoja. Lowassa aliondoka madarakani mwaka 2008 na hadi leo mwaka 2015, ufisadi umepungua au umeongezeka? Tegeta Escrow imetokea wakati gani? Mwenyewe alishasema mwenye ushahidi autoe,” alisema Profesa Lipumba.
Akifafanua kuhusu tuhuma za Lowassa, Dk Makaidi alieleza kuwa bila wasiwasi, anaweza kusema Lowassa ni mwananchi safi na kudai kuwa kama ni mtu mbaya, kwa nini hajashitakiwa na kutupwa jela.
Akifafanua chama atakachojiunga nacho Lowassa, Profesa Lipumba alisema atachagua mwenyewe chama anachokitaka na kuwa kila chama ndani ya Ukawa kitafuata taratibu na kanuni zake katika uteuzi wa mgombea wao wa urais, na mwishoni, Ukawa itasimamisha mgombea wa Urais mmoja kwa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgombea mmoja kwa makubaliano katika ubunge, uwakilishi na udiwani.
Hata hivyo, inaaminika kuwa Lowassa aliyetupwa nje katika kinyang’anyiro cha uteuzi wa Mgombea Urais wa CCM ambacho Dk John Magufuli alishinda, atajiunga na Chadema na kuwa Mgombea Urais wa Ukawa.
“Lazima tufuate taratibu, kwa Ukawa, vyama vitafuata taratibu zake za Katiba, mabaraza ya uamuzi na mikutano yao mikuu…mwanzoni mwa mwezi Agosti tutapata mgombea mmoja na wote tutamuunga mkono,” alisema Profesa Lipumba na kusisitiza azma yake kugombea kupitia CUF.
Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar, Dk Duni Haji akizungumza nje ya mkutano huo alisema hakuna cha ajabu kwa Lowassa kujiunga na Ukawa licha ya huko nyuma kutuhumiwa kwa ufisadi, akitetea kwa kueleza kuwa hivi sasa CUF imeunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwa kushirikiana na mpinzani wake mkuu, CCM.
“Mimi nawashangaaa sana…mnauliza kwa nini Lowassa aje Ukawa. Zanzibar watu waliuawa kule, lakini leo tuko katika Serikali. Angalia Afrika Kusini mfano wa Mandela (Nelson) au Msumbiji kwa vyama vya Frelimo na kile kingine. Wakati fulani hapa, Chadema walisema CUF ni CCM B, lakini leo tuko pamoja. “Katika siasa hakuna adui wa kudumu wala rafiki wa kudumu, kuna kutetea hoja inayouzika. Mwacheni Mzee Lowassa aje tuiondoe CCM, tumechoka kuonewa,” alisema Duni.
Hata hivyo, katika kujibu maswali ya waandishi wa habari, si Mbowe wala Makamu wake Zanzibar, Said Issa Mohammed aliyejibu maswali hayo licha ya baadhi kuelekezwa kwao, na badala yake waliojibu ni Profesa Lipumba, Mbatia na Dk Makaidi.
Maswali mengine yalihusu kauli iliyowahi kutolewa na Chadema kuwa Lowassa ni dhaifu, je atakuwa imara akiwa Ukawa; vipi kuhusu orodha ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibroad Slaa ya kuwamo kwa Lowassa katika orodha ya mafisadi, je, Lowassa hakuhusika katika Richmond na je ndiye atakuwa Mgombea Urais wa Ukawa.
Lowassa alikuwa miongoni mwa wanaCCM 42 waliochukua fomu ya kuwania kuteuliwa kugombea Urais na miongoni mwa 38 waliorejesha fomu na kupelekwa katika vikao vya uteuzi, lakini hakuwemo katika waliopitishwa na Kamati Kuu na kupigiwa kura na Halmashauri Kuu ya Taifa na kisha Mkutano Mkuu Maalumu mwezi uliopita.
Baada ya Mkutano Mkuu Maalumu kumchagua Dk Magufuli, Julai 12, mwaka huu, mwanasiasa huyo wa siku nchini ndani ya CCM na Serikali, ilielezwa kuwa alikuwa anatafakari hatima yake ndani ya chama tawala, na tangu wakati huo taarifa zikamhusisha na kuhamia Chadema ambako inaelezwa makubaliano ya kumruhusu kuwa mgombea wao yalifikiwa juzi usiku katika kikao kilichofanyika katika hoteli moja maarufu Dar es Salaam.HABARI LEO

No comments