Header Ads

Waziri Ndalichako: Ninawapa wiki moja la sivyo tutavunja mkataba na TBA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amechukizwa na hali ya ujenzi katika Hosteli za Chuo Kikuu cha Taaluma na Tiba cha Mloganzila na kuipatia wiki moja Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA) kuhakikisha inarekebisha mapungufu yote.

Profesa Ndalichako ameyasema hayo leo Jumamosi wakati wa ziara ya kukagua hali ya ujenzi Mloganzila, ambapo alishuhudia  ujenzi huo ukiwa umesimama huku kukiwa na uchimbaji wa msingi pekee katika majengo manne.

Amesema hajaridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo, licha ya yeye kutoa kiasi cha Sh3.9 bilioni Agosti mwaka jana kwa ajili ya ujenzi huo wa majengo saba ambayo yangehusisha mabweni mawili ya wanafunzi, jengo la kufundishia, jengo la maktaba, bwalo la chakula, jengo la maabara, jengo la maabara maalum na jengo la kazi za nje.

"Hamko makini na kazi yenu, niwahakikishie ikifika Jumamosi sijaona kinachoendelea nawachukulia hatua haiwezekani nimewapa fedha tangu Agosti mwaka jana mpaka leo mmenichimbia msingi pekee, nahangaika ujenzi ukamilike madaktari wakae hapa watoe huduma kwa wagonjwa ninyi mnaleta mchezo, nipo kazini lazima mtii ninachokiagiza," aling'aka Profesa Ndalichako.

Meneja wa TBA Kanda ya Dar es Salaam, Manasseh Shekalaghe amesema kilichokwamisha ujenzi huo ni mvua zilizonyesha ambazo zilileta changamoto na hivyo msingi ulifukiwa na udongo.

No comments