KATAA KUWA MTI.
Na Paul William
Leo ni siku ya 19 tangu mwaka huu uingie,yapo mengi
tumeshuhudia katika kipindi hiki kifupi yakiendelea katika Nyanja za
siasa,kijamii na hata kiuchumi lakini si lengo langu hasa kuzungumzia masuala
ya kisiasa bali nataka niongee na maisha yako moja kwa moja.
Inawezekana yapo mambo na mipango mingi uliyojiwekea katika
mwaka huu kwamba mpaka kufikia disemba uwe umekamilisha,ni jambo zuri kabisa
wala sikatai lakini shida yangu inakuja pale ambapo tumekuwa watu wa kuweka
mipango yetu na malengo iwe ya muda mrefu au ya muda mfupi na kujikuta muda
tuliojiwekea unakwisha bila kufanya lolote.
Binafsi ni mhanga wa hilo kwa muda mrefu lakini nimekaa na
kuwaza sana ni kwa nini inakuwa hivi!! Ndipo nilipogundua jambo moja baada ya
kukaa na kutafakari KWA MUDA MREFU NIMEKUWA MTI ndio “mti” wengi wetu tumebaki
palepale licha ya mazingira kubadilika.
BAADHI YA SIFA ZA MTI
Mti ni mmea ambao una sifa nyingi,ikiwemo kujitafutia chakula
chake wenyewe,kutafuta mwanga(ukiweka mmea kwenye giza utaona unapinda kuelekea
mwanga ulipo)
Pamoja na sifa zote za mti ama mmea utashangaa kuwa huwa
unafanya mambo yote haya huku ukiwa palepale shina haliwezi kuhama. Ndivyo
ilivyo katika maisha ya baadhi ya wengi wetu ,tumekuwa watu wa kuzungumza na si
kuchukua hatua ama tunaona mambo hayaendi sawa pale tulipo tunaendelea kung’ang’ana
kama mti badala ya kujongea kutafuta fursa nyingine,Mfano mzuri ni kwa mtu
aliyeajiriwa katika kampuni Fulani mshahara mdogo,matusi na masimango toka kwa
mabosi wake na mambo mengine kama hayo lakini utashangaa mtu huyu yupo palepale
leo ni mwaka wa kumi na maisha yake hayasongi kisa anaogopa akiacha kazi hiyo
atahangaika na kitaa.! Matokeo yake ameishia kuwa mtu wa mawazo na vidonda vya tumbo visivyoisha huku familia na
watoto wakimtazama na matokeo yake vifo vya ghafla kabla ya wakati.
Ndugu yangu mimi binafsi tangu nimalize kidato cha nne
nimekuwa mtu wa kuhangaika huku na kule nikitafuta kuajiriwa nilianza na ajira
migodini nikaacha,nikaja katika mambo ya kufundisha shuleni English medium nikaacha na sasa nipo
katika redio,lakini kote ambako nimepita hali ni ileile;
Kwanza mshahara hautoshi,pili masimango toka kwa mabosi
lakini pia kukosa uhuru wa kufanya mambo yangu binafsi.Ndipo nimekaa chini
nakujiuliza sana nikagundua hakuna nililofanya zaidi ya kununua kitanda na
kiwanja na kuishia katika kutimiza mahitaji madogo kama chakula na kodi ya
nyumba huku nikiendelea kuwa mtumwa wa watu,nilikumbuka msemo usemao “UKISHINDWA
KUTIMIZA NDOTO ZAKO,UTAAJIRIWA KUTIMIZA NDOTO ZA WENGINE”
Mwenzenu NIMEKATAA KUWA MTI nimeamua kuchukua hatua na
kuachana na masuala ya kuajiriwa na kuamua kufanya biashara zangu mwenyewe.
Unaweza kupatwa na adha katika eneo lako la kazi kama
kusingiziwa,kunyanyaswa ama hata kufukuzwa,nataka nikuambie kuwa Mungu akitaka
kukuinua kukupeleka hatua nyingine huwa hana namna zaidi ya kukung’oa kwa nguvu
pale ulipo kupitia hao hao ulio nao.
Nikutakie siku njema na wikendi njema lakini kumbuka hili
siku zote “UKITAKA KUFANIKIWA KATIKA MAISHA YAKO,KATAA KUWA MTI”
Post a Comment