Header Ads

Waandishi watabiriwa vifo 2017



MWAKA 2017 huenda ukawa mbaya kwa upande wa waandishi wa habari baada ya utabiri kuonyesha vifo vilivyoikumba tasnia ya habari mwaka jana duniani kote utaendelea mwaka huu.

Aidha, viongozi wakubwa wa upinzani duniani ikiwamo Tanzania wametabiriwa kurejea kwenye vyama walivyovihama mwaka huu.

Utabiri huo ulitolewa jana na mtabiri Maalimu Hassani Yahya Hussein ambaye ni mtoto wa Sheikh Yahya Hussein aliyekuwa mnajimu wa kimataifa ambapo ametoa utabiri huo wa mambo 20 yatakayotokea mwaka huu.

Mtabiri huyo pia alikitabiria kifo chama kimoja cha upinzani maarufu hapa nchini na anguko la vyama tawala katika nchi mbalimbali duniani.

“Chama Cha Mapinduzi kitashika hatamu zaidi itakayoleta maendeleo makubwa pia kuimarika kwa hali ya uchumi duniani kote ikiwamo Tanzania na hali ngumu iliyokuwapo mwaka jana kutoweka.

“Natabiri Rais Dk. John Magufuli kupata nishani ya juu ya dunia kutoka kwa Rais wa moja ya mataifa makubwa duniani kutokana na uongozi wake,” alisema Maalimu Hassan.

Alisema kutatokea mvutano wa kimtazamo na sera utakaosababisha mabadiliko makubwa ya uongozi wa kiserikali duniani na Tanzania ikiwamo ambapo  baadhi ya wanasiasa watapotea kabisa katika ulingo wa siasa.

Pamoja na mambo mengine, alisema mwaka huu huenda ukawa mbaya kwa viongozi baada ya utabiri kuonyesha kuwa viongozi wa dini, kisiasa na wasanii maarufu kuendelea kukumbwa na kashfa za ngono na ulevi zitakazosababisha anguko lao.

Kwa mujibu wa utabiri huo, viongozi wa tasnia ya sheria kwa maana ya wanasheria mawakili na majaji watakumbwa na kashfa hiyo.

“Natabiri kuwapo kwa vifo vya kawaida na ghafla vya wasanii maarufu duniani ikiwamo Tanzania vitakavyotokana na fumanizi kuuliwa au kuuana wenyewe, pia kashfa hizo zitawahusu viongozi wakubwa wa dini, siasa na wasanii maarufu.

“Pia kutawapo kwa majanga ya moto na mafuriko hapa nchini na duniani kote itakayosababisha madhara makubwa ikiwamo vifo na madhara mengine na pia kutakuwa ongezeko la kuibuliwa kwa vitendo vya ufisadi na rushwa,” Alisema.

Alisema mwaka huu unawataliwa na nyota ya Simba unaashiria vifo vya viongozi wakubwa na maarufu wa kidini na kisiasa vitakavyotokea kutokana na msongo wa mawazo au shinikizo la damu.

“Natabiri kuzama kwa meli kwenye moja ya bahari kuu za dunia na ndege moja ya taifa kubwa duniani kuanguka na kusababisha vifo vya watu kadhaa,” alisema Maalimu Hassan.

Alisema ili kuepuka majanga hayo yasitokee watu waache chuki, ubinafsi, choyo, kuchongeana na ngono isiyokubalika kisheria hasa kwa watawala.

No comments