OBAMA AMWAGA MACHOZI AKIWAAGA WAMAREKANI.
Rais wa Marekani, Barack Obama amewaaga Wamarekani na ulimwengu mzima kwa ujumla ikiwa ni mara ya mwisho akiwa kama rais, katika hotuba iliyojaa hisia kubwa aliyoitoa mjini Chicago na kuwataka Wamarekani kuunganisha nguvu katika kuleta mabadiliko.
Rais huyo ametokwa na machozi wakati akimshukuru mke wake Michelle Obama kwa namna alivyotoa mchango mkubwa katika utawala wake.
Akihitimisha utawala wake katika Ikulu ya Marekani, Obama amerejea katika mji ambao sasa ni nyumbani kwake wa Chicago ambako kampeni yake ya "ndio tunaweza" ilianzia hapo na leo akisema "ndio tumeweza".
Akiorodhesha mafanikio ya utawala wake kuanzia mkataba wa nyukilia na Iran hadi huduma ya bima ya afya, sehemu kubwa ya hotuba yake iliegemea katika kuwatia moyo wafuasi wake waloshtushwa na ushindi wa Donald Trump pamoja na kutathmini mafanikio aliyoyapata katika uongozi wake na mtazamo wake kuhusu wapi Marekani inaelekea .
Obama amewataka Wamarekani kuamka, kupigania demokrasia lakini akaonya kuwa ubaguzi wa rangi na kukosekana kwa usawa bado ni kitisho kwa demokrasia.
"Sisi sote bila ya kujali vyama, ni lazima turudi katika ujenzi wa taasisi ya demokrasia", amesema Obama.
"Hivyo sisi kama wananchi, lazima tuwe macho dhidi ya uchokozi wa nje, ni lazima tuilinde misingi yetu inayodhoofika inayotutambulisha sisi ni akina nani. Ndio maana katika kipindi cha miaka nane iliyopita nimefanya kazi ya kuweka mapambano dhidi ya ugaidi katika misingi ya kisheria.
"Ndio maana tumemaliza mateso, kufanya kazi kulifunga gereza la Guantanamo, na mageuzi ya sheria zetu zinazosimamia ufuatiliaji wa kulinda faragha na uhuru wa raia. Na ndio maana mimi nimekataa ubaguzi dhidi ya Waislamu Wamarekani", amenukuliwa rais huyo.
Miongoni mwa mafanikio mengine anayojisifia Obama ni pamoja na kuimarishwa kwa uchumi, kuhalalisha ndoa za jinisia moja, kufunguliwa kwa mahusiano ya kidiplomasia na Cuba na maenedeleo mengine.
Mke wake Michele Obama na makamu wa rais Joe Biden na mke wake Jill ambao rais amewaelezea kama "familia" wamehudhuria hafla hiyo.
Obama akifuta machozi machoni mwake amemshukuru mke wake Michelle akimuita ni rafiki yake mkubwa, mtoto wake Malia aliyekuwa akibubujikwa na machozi pamoja na Sasha ambaye hakuwepo.
Akielezea mchango wa mke wake, Obama anasema, "Michelle Lavaughn Robinson, msichana kutoka upande wa kusini, kwa miaka zaidi ya 20 iliyopita, umekuwa sio tu mke wangu na mama wa watoto wangu lakini rafiki yangu mkubwa.
"Ulichukua jukumu ambalo hukuuliza na ukalifanya kuwa lako kwa neema , ujasiri, mipango na ucheshi mzuri. Uliifanya Ikulu kuwa sehemu ya kila mtu."
Anasema Marekani imekua bora na yenye nguvu duniani tangu alipokula kiapo kuiongoza nchi hiyo miaka nane iliyopita.
Donald Trump atakayeapishwa Januari 20 anatarajiwa kuondoa baadhi ya yaliyofikiwa na karibu kiasi ya watu elfu 18 waliohudhuria hafla hiyo mjini Chicago walimshangilia rais huyo wakisema "miaka minne zaidi" na Obama akasema hawezi kufanya hivyo.
Obama katika hotuba yake ya mwisho ameepuka kumkosoa Trump moja kwa moja na kulaani mgawanyiko ambao umezikumba siasa za taifa hilo.
Imeandikwa na Mtandao wa DW
Michelle Obama akimliwaza binti yake Malia ambaye alijikuta akitokwa na machozi wakati akisikiliza hotuba ya baba yake Rais Barack Obama
Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden naye alijikuta akishindwa kujizuia na kutokwa na machozi
Rais wa Marekani, Barack Obama akikumbatiana na Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden baada ya kumaliza hotuba yake.
Michelle Obama akimkumbatia mumewe rais Barack Obama baada ya kumaliza hotuba yake.
Rais wa Marekani Barack Obama akimkumbatia binti yake Malia baada ya kumaliza hotuba yake.
Post a Comment