Header Ads

MUUGUZI ATUHUMIWA KUSABABISHA KIFO CHA MAMA MJAMZITO HOSPITALI YA RUFAA MKOANI WA MARA.


Uongozi wa hospitali ya rufaa mkoani Mara,umeingia katika tuhuma nyingine baada ya kudaiwa kufanya uzembe na sababisha kifo cha mwanamke mmoja mjamzito Bi Mkami Mirumbe mkazi wa kijiji cha Kinesi wilayani Rorya kwa madai kuwa mmoja ya wauguzi aliomba rushwa ya shilingi laki mbili na baada ya kukosekana kwa kiasi hicho anadaiwa kushindwa kumpatia huduma na hivyo kusababisha kifo chake.

Baadhi ya ndugu wakiongozwa na mama mzazi wa marehemu Bi Fatuma Mirumbe, wamesema baada kumfikisha mgonjwa huyo katika hospitali hiyo ya rufaa mjini Musoma majira ya saa 4 asubuhi akitokea zahanati ya Kinesi,akilalamika kuumwa tumbo na kushindwa kupata haja ndogo kisha kulazwa katika wodi namba moja,ameshindwa kupata huduma kwa zaidi ya saa tatu baada kudaiwa kuwa ya mmoja ya wauguzi katika wodi hiyo kudai kuomba rushwa hiyo ya shilingi laki mbili.

Wamesema baada mgonjwa huyo kufikishwa katika wodi hiyo namba moja, muuguzi huyo aliomba rushwa hiyo ya shilingi laki mbili ili aweze kumtafuta daktari kwa ajili ya kutoa huduma,lakini licha ya ndugu hao kuomba kutoa kiasi cha shilingi 115,000 zilizochangwa na wana ndugu,muuguzi huyo anadaiwa kukataa kupokea kiasi hicho cha fedha kwa kutaka shilingi laki mbili hatua ambayo ilisababisha mgonjwa huyo kukosa huduma na kufariki dunia majira ya saa nane mchana.

Hata hivyo kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Mara Dkt. Nila Jackson,amesema hakuna uzembe ambao umesababisha kifo cha mama huyo mjamzito, huku akisikitishwa na kifo hicho cha ghafla ambacho amedai kimesababisha wananchi kuvamia hospitali na kutaka kuwashambulia wauguzi.
Kwasababu hiyo katibu tawala wa mkoa wa Mara Bw Adoh Mapunda,amesema baada ya kupata malalamiko hayo,tayari ameandika barua kwa kutaka uongozi wa hospitali kutoa maelezo juu ya kifo hicho ikiwa ni pamoja kuunda tume kuchunguza tuhuma hizo.

No comments