Header Ads

FALSAFA MPYA YA MAISHA; Unawezaje Kuwa Mtu Mzuri?

Ni matumaini yangu kuwa haujambo msomaji wangu wa blog hii na jumapili ya leo imekuwa njema sana kwako.
Leo tutakwenda kuangalia eneo muhimu sana la maisha yetu. Eneo hili wengi wamekuwa wakiona haya kulizungumzia moja kwa moja. Lakini sisi kama wanafalsafa, tunahitaji kulizungumzia eneo hili bila ya hofu yoyote kwa sababu tunahitaji kuyaboresha maisha yetu.
Tunachokwenda kuzungumzia leo ni jinsi gani unakuwa mtu mzuri. Na kabla sijaendelea naomba niseme kwamba uzuri tunaozungumzia hapa siyo urembo au utanashati, bali uzuri wa mtu, kama mtu. Na pia siyo wema ambao unaweza kuchagua kumfanyia mtu, hapa tunazungumzia uzuri wa mtu. Je unawezaje kuwa mtu mzuri?
Kabla hatujaangalia uzuri wa mtu ni nini na tunawezaje kuwa watu wazuri, tuangalie mifano ya asili kabisa kuhusu uzuri.
Unasemaje huyu ng’ombe ni mzuri? Unasema ng’ombe ni mzuri pale anapofanya mambo ambayo tunategemea ng’ombe ayafanye, na akayafanya kwa kiwango cha hali ya juu. Tunategemea ng’ombe atoe maziwa, ng’ombe akitoa maziwa mengi tunasema ng’ombe huyu ni mzuri. Tunategemea atoe nyama, akitoa nyama nyingi na nzuri tunasema ni mzuri.
Tunasemaje huu mwembe ni mzuri? Tunapima uzuri wa mti wa embe kwa kile ambacho unazalisha. Kama utatoa maembe makubwa na matamu tutasema huu mwembe ni mzuri na tutafurahia kuwa nao. Tutakata miti mingine kwa ajili ya shughuli zetu, lakini ule mwembe tutauacha, kwa sababu ni mzuri kwetu.
Katika mifano hiyo miwili hapo juu umejifunza nini? Kikubwa utakachoona hapo, ni kwamba uzuri wa kitu unapimwa kwa thamani ambayo kitu hicho kinatoa kwa wengine. Pale kitu kinapotoa kile ambacho inatarajiwa kutoa, na ikatoa kwa ubora basi tunasema kitu hicho ni kizuri.
Sasa turudi kwetu sisi binadamu. Unasemaje mtu ni mzuri? Ni sifa zipi unatumia kusema huyu ni mzuri na yule mbaya?
Kama ilivyo kwa vitu vingine, kipimo kikubwa cha uzuri ni ile thamani ambayo mtu anatoa kwa wengine. Pale mtu anapofanya kile ambacho anatarajiwa kufanya, na akakifanya kwa ubora, basi huyo tunasema ni mtu mzuri.
Hivyo kama unataka kuwa mtu mzuri, na kila mwanafalsafa lazima awe mtu mzuri, lazima ufanye kile unachotegemewa kufanya kama mtu na kifanye kwa ubora kiasi kwamba unaongeza thamani kwenye maisha yako.
Ni mambo gani ambayo mtu anategemewa kufanya?
  1. Kuwa na kazi au shughuli inayotoa mchango kwa wengine.
Kila mtu anategemewa awe na shughuli ambayo inatoa mchango kwenye maisha ya wengine. Iwe ni ajira au biashara, lazima uwe na kitu ambacho watu wanakitegemea ili kuwa na maisha bora. Hivyo huwezi kuwa mtu mzuri kama hakuna unachofanya kwa ajili ya wengine.
  1. Nenda hatua ya ziada kwenye kile unachofanya.
Kuna kiwango ambacho unategemewa kufanya, na kila mtu anafanya hivyo. Unapokwenda zaidi ya kiwango hicho, kuhakikisha unatoa thamani kubwa kwa wengine, hapo unakuwa mtu mzuri. Unapokuwa tayari kutoa zaidi kwa wengine, unakuwa mtu mzuri. Kama ambavyo ng’ombe anayetoa maziwa mengi ni mzuri kuliko anayetoa maziwa kidogo.
  1. Mpende kila mtu bila ya masharti.
Sifa nyingine ya uzuri ni kuwapenda wengine, wapende watu kama walivyo, bila ya masharti au vigezo vyovyote. Wapende watu kwa sababu ni binadamu, na hakuna kitu watu wanapenda kama kupendwa. Usiweke masharti ya kipato au urembo katika kuwapenda watu, wapende vile walivyo, kwa kuthamini kile wanachofanya.
  1. Wajali wengine.
Kupenda peke yake haitoshi, unahitaji kuwajali wengine. Kuwapa muda wengine, kuwasaidia katika changamoto wanazopitia. Unapowasaidia wengine wakawa na maisha bora ndivyo unavyokuwa mtu mzuri.
  1. Toa bila ya kutegemea kupokea.
Msingi wa maisha ni kutoa, kabla hata hujafikiria kupokea. Lakini jamii zetu zimekuwa zinatufundisha mbinu za kupokea pekee, na hivyo kuharibu mahusiano yetu na wengine. Mara nyingi pia tumekuwa tunafundishwa kutoa ili tupokee, hivyo tunatoa, halafu tunatumia tulichotoa kulazimisha kupokea. Kwamba nipe kitu fulani kwa sababu mimi nilikupa kitu fulani. Hii haikufanyi kuwa mtu mzuri. Mtu mzuri ni yule anayetoa, bila ya kutegemea kupokea, anatoa kwa sababu ndiyo kitu alichonacho na atategemewa kukitoa. Na kwa kuwa kanuni za asili zinafanya kazi, lazima atapokea, ila siyo yeye anayedai kupokea.
Kwa mfano, kama umekula tunda lolote leo, kuna mti wa tunda hilo ambao umekuambia ndizi uliyokula nimetoa mimi? Au kama umekunywa maziwa, kuna ng’ombe amekufuata na kukuambia maziwa uliyokunywa nimetoa mimi? Hakuna, umefurahia vitu hivi kwa sababu kuna kitu kimetoa, na wewe umekuwa tayari kutoa fedha kupata kitu hicho, siyo kwa sababu umelazimishwa, ila kwa sababu umepata thamani.
Anza na wewe kutoa, toa kwa sababu unatoa, na siyo kwa sababu unataka kupokea. Utakuwa mtu mazuri na maisha yako kuwa bora.
Je ni yapi unayofanya ili kuwa mtu mzuri?
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,

No comments